News

BARABARA SUMBAWANGA–MATAI–KASESYA KUFUNGUA LANGO JIPYA LA BIASHARA TANZANIA–ZAMBIA

Ujenzi wa Barabara ya Sumbawanga–Matai–Kasesya unaendelea katika Mkoa wa Rukwa, huku kukamilika kwa mradi huo kukitarajiwa kuimarisha usafirishaji wa mizigo, kuchochea biashara na kufungua fursa mpya za kiuchumi kati ya Tanzania na Zambia.

Kaimu Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Ngereja Joshua, amesema mradi huo unatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani kutoka Serikali ya Tanzania (GOT), huku Kampuni ya China Geo ya China ikiwa Mkandarasi anayesimamia utekelezaji wa ujenzi, na usimamizi wa mradi ukifanywa na kitengo cha Usimamizi wa Miradi (TECU).

Kwa mujibu wa Mhandisi Ngereja, barabara hiyo ni miongoni mwa miradi muhimu ya kimkakati kwa Mkoa wa Rukwa na Taifa kwa ujumla, kutokana na nafasi yake ya kuunganisha Mkoa wa Rukwa kupitia Wilaya ya Kalambo na nchi jirani ya Zambia. Amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutaimarisha mawasiliano na usafirishaji wa mizigo, huku kukifungua fursa zaidi za biashara na shughuli za kiuchumi kati ya Tanzania na Zambia.

“Barabara hii ni muhimu kwa sababu itaongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo kati ya Tanzania na Zambia, sambamba na kufungua fursa zaidi za biashara kwa wananchi na wafanyabiashara wa pande zote mbili,” amesema Mhandisi Ngereja.

Aidha, amesema barabara hiyo itakuwa njia mbadala ya usafirishaji wa mizigo, hatua inayotarajiwa kupunguza utegemezi wa njia ya Tunduma na hivyo kusaidia kupunguza msongamano katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Miradi ya Maendeleo wa TANROADS Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Joseph Gimonge, amesema kipande cha barabara cha Katanda–Kasesya chenye urefu wa kilomita 25, ambacho ni sehemu ya Barabara ya Matai–Kasesya, kinatarajiwa kukamilika ifikapo Agosti 2027.

Mhandisi Gimonge amesema mradi huo tayari umeanza kutoa manufaa kwa wananchi wa Mkoa wa Rukwa kupitia ajira, ambapo jumla ya ajira 162 zimetolewa kwa wazawa wanaoshiriki katika utekelezaji wa mradi huo.

Amesema uwepo wa mradi huo unatoa fursa kwa wananchi kushiriki moja kwa moja katika shughuli za ujenzi, huku ukichangia pia ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika maeneo yanayozunguka mradi.

TANROADS Mkoa wa Rukwa, kwa kushirikiana na TECU, inaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha ujenzi unafanyika kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa na kukamilika ndani ya muda uliopangwa.

Kukamilika kwa barabara ya Sumbawanga–Matai–Kasesya kunatarajiwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha mtandao wa usafirishaji, kukuza biashara ya mipakani na kuongeza fursa za kiuchumi kwa Tanzania na Zambia.