MIZANI YA MINGOYO KUSINI YAIMARISHA ULINZI WA MIUNDOMBINU YA BARABARA MKOA WA LINDI
Lindi, 17 Julai, 2026
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) unaendelea kuimarisha usimamizi wa uzito wa magari kupitia Kituo cha Mizani cha Mingoyo Kusini mkoani Lindi, hatua inayolenga kulinda miundombinu ya barabara na kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara.
Msimamizi wa Mizani Mkoa wa Lindi, Mhandisi Godfrey Kallanga, amesema kituo hicho hupima magari yanayosafiri kati ya mikoa ya Lindi na Mtwara kwa kuzingatia Sheria ya Mizani ya Afrika Mashariki, ili kuhakikisha yanakidhi viwango vya uzito vinavyoruhusiwa.
Ameeleza kuwa magari yanayobainika kuzidisha uzito hutozwa faini kulingana na kiwango cha uzito uliozidi, kwa uzito wa jumla wa gari (GVM) au uzito wa ekseli (Axle Load), baada ya kulipa faini, dereva hutakiwa kupanga upya au kupunguza mzigo, kisha gari hupimwa tena kabla ya kuruhusiwa kuendelea na safari.
Kwa sasa, kituo hicho hupima magari kati ya 400 na 600 kwa siku, huku wastani wa magari yanayobainika kuzidisha uzito ukishuka hadi matatu au manne kwa siku.
Mhandisi Kallanga amesema hali hiyo inadhihirisha kuwa kumekuwa na ongezeko la uelewa na uzingatiaji wa sheria za udhibiti wa uzito wa magari, ambapo inasaidia kuongeza maisha ya barabara na kupunguza gharama za matengenezo.
Naye dereva wa lori, Ali Salum Jalo, amesema mizani ina mchango mkubwa katika kulinda barabara na kuimarisha usalama wa usafiri kwa kuhakikisha magari yanabeba mizigo inayoruhusiwa kisheria, hivyo kupunguza uharibifu wa miundombinu na hatari ya ajali.