MAWAZIRI WA EAC WAAZIMIA KUHARAKISHA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA KIMKAKATI YA MIUNDOMBINU
Arusha, 10 Julai, 2026
Mawaziri wanaosimamia sekta za Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameazimia kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya miundombinu ya barabara, reli, usafiri wa anga na viwanja vya ndege, usafiri wa majini pamoja na sekta ndogo ya mawasiliano ili kuimarisha mtangamano wa kikanda, kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha ustawi wa wananchi.
Azimio hilo limefikiwa katika Mkutano wa 20 wa Baraza la Kisekta la Uchukuzi, Mawasiliano na Hali ya Hewa (TCM) la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika Julai 10, 2026, katika Makao Makuu ya Jumuiya jijini Arusha.
Mkutano huo umejadili hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa maamuzi ya mkutano uliopita wa TCM, hususan kuhusu miradi na programu za kikanda katika sekta za barabara, reli, usafiri wa anga na viwanja vya ndege, usafiri wa majini pamoja na mawasiliano.
Akifungua mkutano huo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Mhandisi Godfrey Kasekenya (Mb), alisema kuwa miundombinu ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na nguzo muhimu katika kuimarisha mtangamano wa nchi wanachama, kuvutia uwekezaji, kuongeza fursa za ajira na kuboresha mazingira ya biashara.
“Sote tunatambua kuwa sekta za barabara, reli, usafiri wa anga na mawasiliano ni msingi wa maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi wetu. Aidha, sekta hizi zina mchango mkubwa katika kuongeza ushindani wa nchi zetu na Jumuiya, katika soko la kikanda na kimataifa,” alisema Mhe. Mhandisi Kasekenya.
Miongoni mwa miradi ya kimkakati iliyopewa kipaumbele ni ujenzi wa barabara za Masaka–Mutukula/Mutukula–Kyaka, Bugene–Kasulo–Kumunazi, Malindi–Mombasa–Lunga Lunga/Tanga–Bagamoyo, Nyakanazi–Kasulu–Manyovu/Rumonge–Bujumbura, Arusha–Holili–Mwatate, Lusahunga–Rusumo/Kayonza–Kigali, pamoja na utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa ujenzi wa Vituo vya Huduma Pamoja Mipakani (One Stop Border Posts - OSBPs).