News

Mtendaji Mkuu wa TANROADS Aagiza Kuongeza Kasi ya Ujenzi wa Barabara ya Arusha–Kibaya–Kongwa

Mtendaji Mkuu wa TANROADS Aagiza Kuongeza Kasi ya Ujenzi wa Barabara ya Arusha–Kibaya–Kongwa

Arusha, 06 Julai 2026

Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, ameagiza Mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Barabara ya Arusha–Kibaya–Kongwa, sehemu ya Mbauda–Losinyai na T/Packers (Moshono)–Losinyai, ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotarajiwa.

Maelekezo hayo yalitolewa wakati wa kikao kazi cha ngazi ya juu kilichofanyika hivi karibuni kiliwakutanisha viongozi wa TANROADS na Mkandarasi kwa lengo la kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa mradi na kujadili mikakati ya kuharakisha kazi. Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Mhandisi Regnald Massawe. 

Mradi huo wenye urefu wa kilomita 70 ulianza kutekelezwa mwezi Aprili 2026 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 222, ukigharamiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mradi unahusisha ujenzi wa barabara ya njia nne katika eneo la Mbauda–Arusha Bypass, pamoja na ujenzi wa barabara kutoka Kona ya Mrombo kupitia Bondeni City, Oljoro, Losinyai, Loki na Kiserian hadi T/Packers (Moshono) kwa njia mbili.

Katika kikao hicho, Mtendaji Mkuu alisisitiza umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wa kazi, hususan katika maeneo yatakayohudumia watumiaji wengi wa barabara na shughuli mbalimbali za kitaifa, ikiwemo maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), aidha, alielekeza Mkandarasi kuongeza wafanyakazi, mitambo na kuendesha shughuli za ujenzi kwa zamu za mchana na usiku ili kuhakikisha ratiba ya mradi inazingatiwa. 

Vilevile, Mkandarasi alielekezwa kuhakikisha upatikanaji wa vifaa muhimu vya ujenzi, ikiwemo lami, ili kuondoa uwezekano wa ucheleweshaji wa utekelezaji wa mradi. TANROADS itaendelea kufanya vikao vya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati. 

Mhandisi Besta, pia alitoa wito kwa taasisi zote zinazohusika, zikiwemo Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWASA) na Serikali ya Mkoa wa Arusha, kuendelea kutoa ushirikiano katika kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi. Ushirikiano huo utawezesha kukamilika kwa mradi kwa wakati na kwa viwango vinavyokidhi matarajio ya Serikali na wananchi.