SERIKALI YATANGAZA MIRADI MIKUBWA YA BARABARA KWA UBIA NA SEKTA BINAFSI
Dodoma, 22 Juni, 2026
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema Serikali imeelekeza utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ya kimkakati kufanyika kwa mfumo wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Akichangia Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/2027, Ulega amesema tayari Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) umetangaza fursa za uwekezaji katika miradi mbalimbali ya kimkakati ya barabara kuu na kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kushiriki katika utekelezaji wake.
“Barabara za kimkakati zilizotangazwa kwa ajili ya utekelezaji zitajengwa kwa mfumo wa PPP, hatua ambayo itasaidia kuharakisha maendeleo ya nchi yetu kwa ufanisi zaidi,” amesema Ulega.
Miradi iliyotangazwa ni pamoja na upanuzi wa barabara ya Morogoro–Dodoma (km 260);barabara ya Handeni–Kiberashi–Chemba–Kwamtoro–Singida (km 384); upanuzi wa barabara ya Chalinze–Segera–Tanga (km 246); mradi wa Mteremko wa Kitonga (km 27); barabara ya Mwendokasi (Expressway) ya Dar es Salaam–Kibaha (km 42); na Expressway ya katikati ya Jiji la Dar es Salaam hadi Uwanja wa Ndege wa JNIA (km 10).
Hatua hiyo inaonesha dhamira ya Serikali ya kuweka kipaumbele ushirikiano na Sekta Binafsi katika kuimarisha miundombinu ya usafiri, kuongeza ufanisi wa usafirishaji na kuvutia uwekezaji kwa manufaa ya uchumi wa Taifa.