BARABARA YA TIMBOLO – MIANZINI KUFUNGUA FURSA MPYA KWA WANANCHI WA ARUSHA
Dodoma, 22 Juni, 2026
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Bw. Suleyman Msumi amesema ujenzi wa barabara ya Timbolo – Mianzini yenye urefu wa kilometa 18 unaotekelezwa na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) utaleta manufaa makubwa kwa wananchi kwa kuboresha usafiri, kuchochea biashara na kufungua fursa za kiuchumi katika maeneo yanayohudumiwa na barabara hiyo.
Bw. Msumi ameyasema hayo leo alipotembelea banda la TANROADS katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.
Amesema mradi huo utarahisisha huduma za kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa Arusha, kupunguza muda wa safari, kuongeza thamani ya maeneo ya makazi na biashara pamoja na kusaidia ukuaji wa sekta ya utalii. Utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 56.
Aidha, amesema miradi mbalimbali ya barabara inayotekelezwa na TANROADS mkoani Arusha imeendelea kuboresha maisha ya wananchi kwa kuunganisha maeneo ya uzalishaji na masoko, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuongeza fursa za uwekezaji.
Bw. Msumi amewataka wananchi kuitunza miundombinu hiyo ili iendelee kutoa manufaa ya muda mrefu kwa kizazi cha sasa na kijacho, huku akiipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa inayochochea maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi.
Pia ameihakikishia TANROADS ushirikiano wa Halmashauri ya Arusha katika kulinda na kusimamia miundombinu hiyo ili iendelee kutoa huduma bora kwa wananchi kwa miaka mingi ijayo.