News

TANROADS YACHUKUA HATUA DHIDI YA MAEGESHO HOLELA YA MALORI MBAGALA ZAKHEM

TANROADS YACHUKUA HATUA DHIDI YA MAEGESHO HOLELA YA MALORI MBAGALA ZAKHEM

Dar es Salaam, 07 Juni, 2026

Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Lazeck Kyamba katika operesheni ya kuzuia maegesho holela ya malori amesema kumekuwa na ongezeko la malori yanayotumia barabara hiyo kusimama katika eneo la Mbagala Zakhem yanayoathiri shughuli mbalimbali za usafirishaji zinazoendelea.

Mhandisi Kyamba amesema uegeshaji huo holela umekuwa ukichangia msongamano wa magari na kuhatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara hiyo.

Amesema kuwa baadhi ya madereva wamekuwa wakiegesha malori katika maeneo yasiyoruhusiwa, ikiwemo kwenye barabara saidizi (service road), jambo ambalo linaathiri matumizi sahihi ya miundombinu ya barabara na kusababisha usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara.

Kutokana na hali hiyo, TANROADS imeendesha operesheni maalum ya kuondoa malori yaliyokuwa yameegeshwa kinyume na taratibu pamoja na kutoa elimu kwa madereva kuhusu umuhimu wa kutumia maeneo yaliyotengwa rasmi kwa ajili ya maegesho ya magari makubwa.

Aidha, madereva wamehimizwa kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani kwa kuepuka kuegesha magari katika maeneo yasiyoruhusiwa, ili kulinda miundombinu ya barabara na kuhakikisha usalama wa watumiaji wote wa barabara.

Mhandisi Kyamba amesisitiza kuwa operesheni hizo zitakuwa endelevu na zitaendelea kufanyika mara kwa mara ili kuhakikisha sheria za matumizi ya barabara zinazingatiwa na kuondoa changamoto zinazotokana na maegesho holela ya malori.

“Lengo letu ni kuhakikisha barabara zinatumika kwa usalama, ufanisi na kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa, tunawaomba madereva wote kushirikiana nasi kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika.” amesema Mhandisi Kyamba.