News

KWAGILWA AIPONGEZA WIZARA YA UJENZI NA TANROADS UHIFADHI WA MAZINGIRA KUPITIA UPANDAJI MITI

KWAGILWA AIPONGEZA WIZARA YA UJENZI NA TANROADS UHIFADHI WA MAZINGIRA KUPITIA UPANDAJI MITI

Dodoma, 01 Juni, 2026

Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa, ametembelea banda la maonesho ya Siku ya Mazingira Duniani 2026 la Wizara ya Ujenzi pamoja na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) yanayofanyika katika Viwanja vya Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Akiwa katika banda hilo leo, Juni 01, 2026 Mhe. Kwagilwa ameipongeza Wizara ya Ujenzi na TANROADS kwa kuendelea kutekeleza utamaduni wa upandaji miti katika miradi ya barabara, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuhifadhi mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, Kwagilwa amesema kuwa Serikali inaelekea kufanya suala la upandaji miti katika miradi ya maendeleo kuwa la kisheria badala ya kutegemea hiari, ili kuhakikisha kuwa miradi yote inayotekelezwa nchini inaambatana na jitihada za uhifadhi wa mazingira.

“Ni muhimu kuhakikisha kuwa kila mradi wa maendeleo unaenda sambamba na upandaji miti ili kulinda na kuboresha mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema Mhe. Kwagilwa.

Awali Kaimu Meneja wa Mazingira na Jamii, Bw. Julius Luhuro amemweleza mgeni kuwa TANROADS wanampango wa kupanda miti 40,000 kwa kila mwaka kwa miradi mbalimbali nchi nzima na pia inahakikisha kwenye kila mradi wanapanda miti ili kurudisha miti iliyokatwa kipindi cha ujenzi.

Pia Bw. Luhuro amesema katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi hususan mvua kubwa zenye kuathiri barabara, sasa katika miongozo na usanifu sasa wameweka kipengele cha mabadiliko ya tabianchi, katika ujenzi wa madaraja na barabara. 

Maonesho hayo yameanza leo tarehe 01 Juni, 2026 na kufunguliwa rasmi na Naibu Waziri huyo, huku yakitarajiwa kuhitimishwa Juni 05, 2026 kwa Mgeni atakuwa Makamu wa Rais, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, ambapo Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu isemayo: “Dira 2050: Tuwajibike Kukijanisha Tanzania.”