News

SERIKALI YASEMA UJENZI WA BARABARA YA TANGA–PANGANI WAFIKIA ZAIDI YA ASILIMIA 50

SERIKALI YASEMA UJENZI WA BARABARA YA TANGA–PANGANI WAFIKIA ZAIDI YA ASILIMIA 50

Dodoma, 21 Mei,2026

Serikali imesema ujenzi wa barabara ya Tanga hadi Pangani kwa kiwango cha lami unaendelea kama ilivyopangwa, huku utekelezaji wa mradi huo ukiwa umefikia zaidi ya asilimia 50.

Kauli hiyo imetolewa bungeni na Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, alipokuwa akijibu swali la Mbunge, Mhandisi Mwanaisha Ulenge, kuhusu maendeleo ya miradi ya barabara katika Mkoa wa Tanga.

Mhandisi Kasekenya amesema barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 50 ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kuboresha miundombinu ya usafiri na kuunganisha Mkoa wa Tanga na maeneo mengine muhimu kiuchumi.

“Mkakati wa Serikali kukamilisha barabara ya Tanga hadi Pangani upo pale pale na unaendelea, na itajengwa kwa lami ikiwa na urefu wa kilometa 50. Kwa sasa tuko zaidi ya asilimia 50 ya utekelezaji,” alisema Kasekenya.

Ameeleza kuwa Serikali pia inaendelea na mpango wa kuunganisha barabara ya Tanga hadi Makurunge mkoani Pwani kupitia Bagamoyo, ambapo ujenzi wa baadhi ya vipande vya barabara hiyo tayari unaendelea.

Aidha, Serikali imesema inaendelea na hatua za awali za upanuzi wa barabara ya Tanga hadi Segera ili kukidhi ongezeko la matumizi ya barabara hiyo kutokana na ukuaji wa shughuli za kiuchumi katika Bandari ya Tanga.

“Kuhusu barabara ya Tanga–Segera, kwa sasa tunatafuta Mhandisi Mshauri ili aweze kuisanifu na kuweza kuipanua, hasa kufuatia mafanikio ya Bandari ya Tanga,” alisema Kasekenya.

Hatua hiyo inatarajiwa kusaidia kuimarisha usafirishaji wa mizigo na kuchochea shughuli za biashara kati ya Mkoa wa Tanga na maeneo mengine ya nchi.