MABORESHO YA UWANJA WA NDEGE MUSOMA KUCHOCHEA UTALII
Mara, 12 Mei,2026
Kukamilika kwa maboresho ya Uwanja wa Ndege wa Musoma kunatajwa kuwa hatua muhimu itakayochochea ukuaji wa sekta ya utalii, biashara na uchumi kwa ujumla katika ukanda wa Ziwa Victoria na mikoa jirani.
Maboresho hayo yanatarajiwa kurahisisha usafiri wa anga kwa watalii wanaotembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo mkoani Mara, hususan Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Musa Kaswahili, amesema uwanja huo umeboreshwa kutoka kiwango cha changarawe kwenda kiwango cha lami, huku urefu wa barabara ya kutua na kurukia ndege ukiongezwa kutoka mita 1,600 hadi mita 1,800.
Aidha, amesema kazi za ujenzi na maboresho zimehusisha barabara ya kutua na kurukia ndege, maegesho ya ndege, ujenzi wa uzio wa usalama pamoja na jengo la zimamoto.
“Uwanja wa Ndege wa Musoma ni kiungo muhimu katika sekta ya utalii, kwani watalii kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi, ikiwemo Kenya na mataifa jirani, hutumia uwanja huu kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,” amesema Mhandisi Kaswahili.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi huo umeleta manufaa makubwa kiuchumi kwa wananchi, hususan kupitia ajira zilizotolewa kwa wazawa wakati wa ujenzi. Pia amesema mradi huo unasimamiwa kwa ufanisi na Kitengo cha Ushauri na Usimamizi wa Kitaalamu wa Miradi cha TANROADS (TECU).
Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Julai mwaka huu na hadi sasa umefikia asilimia 67 ya utekelezaji, huku barabara ya kutua na kurukia ndege ikikamilika kwa asilimia 100.
Halikadhalika, maboresho hayo yanatarajiwa kuongeza idadi ya ndege zinazotua na kuruka katika uwanja huo, jambo litakalosaidia kupunguza changamoto za usafiri na kufungua fursa mpya za uwekezaji katika sekta za hoteli, usafirishaji, biashara ndogo ndogo pamoja na huduma nyingine za kijamii.
Serikali imeendelea kuwekeza katika kuboresha viwanja vya ndege pamoja na miundombinu mingine ya usafiri nchini kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi, kuongeza mapato ya taifa na kuimarisha sekta ya utalii ambayo ina mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania.
Wananchi wa Musoma na maeneo ya jirani sasa wana matumaini kuwa maboresho hayo yataifanya Musoma kuwa kitovu muhimu cha biashara na utalii katika ukanda wa Kaskazini mwa Tanzania.