News

MIRADI YA BRT DAR KUENDELEA KWA KASI; TANROADS YASISITIZA UBORA NA USALAMA KWA WANANCHI.

MIRADI YA BRT DAR KUENDELEA KWA KASI; TANROADS YASISITIZA UBORA NA USALAMA KWA WANANCHI.

Dar es salaam, 9 Mei,2026

Meneja wa Miradi ya BRT 1 na 4 kutoka Wakala ya Barabara Tanzania TANROADS, Mhandisi Allen Natai, ameongoza ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya miradi ya mabasi yaendayo haraka (BRT) jijini Dar es Salaam akiwa ameambatana na wawakilishi kutoka World Bank.

Ziara hiyo imelenga kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayosimamiwa na TANROADS, ikiwemo BRT 1 Sehemu A kutoka Ubungo hadi Kimara, BRT 4 sehemu ya tatu ya mradi wa Mbuyuni, Kituo cha Mabasi cha Kivukoni (Terminal), pamoja na mradi wa BRT 4 eneo la Simu 2000.

Akizungumzia maendeleo ya miradi hiyo, Mhandisi Allen amesema upanuzi wa barabara katika eneo la Kimara umefikia takribani asilimia 75. Amesema mradi huo utahusisha ujenzi wa njia tatu za magari kila upande pamoja na njia maalum za mabasi yaendayo haraka, hatua inayotarajiwa kupunguza msongamano wa magari katika Barabara ya Morogoro.

Aidha, ameeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea vizuri kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa, huku wasimamizi wa miradi wakiendelea kufuatilia kwa karibu kila hatua ya ujenzi ili kuhakikisha kuwa inakidhi malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wa eneo la Simu 2000, Mhandisi Allen amesema ujenzi wa soko la kudumu kwa wafanyabiashara unaendelea kabla ya kuanza kwa hatua nyingine za mradi. Vilevile, katika eneo la Mbuyuni mkandarasi tayari ameanza kazi za awali ikiwemo uwekaji wa uzio wa eneo la mradi.

Sambamba na hilo, amewasihi watumiaji wa Barabara ya Morogoro kuwa waangalifu kutokana na ongezeko la msongamano wa magari unaotokana na shughuli za ujenzi zinazoendelea. Pia amewahimiza wananchi kutumia madaraja ya waenda kwa miguu yaliyowekwa katika maeneo ya Kimara ili kuepusha ajali na kulinda usalama wao.

Kadhalika, amewashukuru wananchi kwa uvumilivu wao katika kipindi chote cha utekelezaji wa miradi hiyo na kusisitiza kuwa Tanzania National Roads Agency itaendelea kusimamia miradi hiyo kwa weledi hadi itakapokamilika kwa mafanikio.