TANROADS MBEYA YAANZA MRADI WA DARAJANI UYOLE YA KATI KUPUNGUZA MSONGAMANO WA MAGARI
Mbeya
Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania(TANROADS) Mkoa wa Mbeya Mhandisi Suleiman Bishanga,amesema serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja jipya katika eneo la Uyole ya Kati,mradi unaolenga kupunguza msongamano wa magari pamoja na kuboresha mtiririko wa usafiri katika eneo hilo lenye shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii.
Amesema,mradi huo unatarajiwa kugharimu takribani shilingi milioni 454 na utahusisha ujenzi wa daraja,barabara unganishi pamoja na uwekaji wa taa za barabarani ili kuongeza ufanisi na usalama wa watumiaji wa barabara.
Kwa mujibu wa Mhandisi Bishanga,daraja hilo litakuwa njia mbadala kwa magari yanayotoka Mlima Nyoka kuelekea maeneo ya Kasumulu,Kyela na Rungwe,hivyo kusaidia kupunguza msongamano mkubwa wa magari yanayopita katika eneo la Uyole ya Kati.
Amefafanua kuwa ujenzi wa mradi huo ni sehemu ya mwendelezo wa jitihada za serikali za kupunguza changamoto ya msongamano wa magari katika Mkoa wa Mbeya,ambapo awali pia ilifadhili upanuzi wa barabara ya Mlima Nyoka uliochangia kwa kiasi kikubwa kuboresha mtiririko wa usafiri.
Aidha,TANROADS Mbeya imeeleza kuwa serikali pia imetoa fedha kwa ajili ya kushughulikia changamoto za barabara katika eneo la Inyala,ambapo mchakato wa kupitia upya usanifu (design) wa barabara unaendelea ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora,salama na za haraka zaidi za usafiri.
Katika hatua nyingine,Mhandisi Bishanga amewataka wananchi kulinda miundombinu ya barabara ikiwemo taa na alama za barabarani,akisisitiza kuwa miradi hiyo inagharimu fedha nyingi za umma na inalenga kuboresha urahisi wa usafiri,usalama barabarani na upatikanaji wa huduma muhimu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.