TANROADS YATHIBITISHA MAENDELEO CHANYA YA MRADI WA BRT 3.
Dar es salaam, 7 Mei,2026
Meneja wa mradi BRT 3 Mhandisi Frank Mbilinyi kutoka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) akiongozana na wawakilishi kutoka World Bank wametembelea na kukagua mradi wa Ujenzi wa Mabasi yaendayo Haraka BRT 03 sehemu ya kwanza na ya pili ya mradi unaotekelezwa jijini Dar es Salaam na kusimamiwa na TANROADS ikiwa ni sehemu ya ziara yao ya kikazi ya kufuatilia utekelezaji wa miradi wanayoisimamia nchini.
Kwa mujibu wa Msimamizi wa Mradi wa Ujenzi wa Mabasi yaendayo Haraka BRT 03, Mhandisi Mbilinyi amesema mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili, sehemu ya kwanza ya mradi kutoka mjini Posta hadi Gongo la Mboto na sehemu ya pili ya mradi ambayo ni ujenzi wa kituo cha Mabasi yaendayo Haraka kilichopo Gongolamboto. Ambapo sehemu ya kwanza inayohusisha ujenzi wa barabara imefikia hatua za mwisho, huku kazi zilizobaki zikiwa ni za ukamilishaji.
Aidha, ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi unaendelea vizuri kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa, huku wasimamizi wa mradi wakiendelea kufuatilia kwa karibu kila hatua ya ujenzi ili kuhakikisha kuwa unakidhi malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wa sehemu ya pili ya mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi yaendayo haraka kilichopo Gongolamboto,Mhandisi Mbilinyi amesema kazi zipo katika hatua za awali ambapo ni asilimia 8,mkandarasi anaendelea na maandalizi pamoja na utekelezaji wa kazi mbalimbali za ujenzi.
Amefafanua kuwa mradi huo wa BRT3 ni muhimu kwa maendeleo ya miundombinu ya usafiri nchini, kwani utaimarisha usafiri katika jiji la Dar es Salaam na kurahisisha usafirishaji wa watu bidhaa, pamoja na kuchochea shughuli za kiuchumi katika maeneo husika.
Aidha, amewashukuru wananchi kwa uvumilivu wao katika kipindi chote cha utekelezaji wa mradi huo na kusisitiza kuwa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) itaendelea kusimamia utekelezaji wake kwa weledi hadi kukamilika kwake kwa miradi hio.