UPEMBUZI YAKINIFU BARABARA YA IPYANA - ILEJE WAFIKA ASILIMIA 96
Dodoma, 06 Mei, 2026
Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imeeleza kuwa inaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Ipyana–Kasumulu–Ngana–Ndembo–Ileje (Isongole) yenye urefu wa kilomita 114.3, ambapo kwa sasa hatua ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina imefikia asilimia 96.
Aidha, ujenzi wa kipande cha Isongole II–Ndembo pamoja na barabara ya kuingia Ndembo–Isoko (km 52) umefikia asilimia 10.75.
Kauli hiyo imetolewa leo, tarehe 6 Mei, 2026, Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kyela, Mhe. Baraka Ulimboka Mwamengo, aliyeuliza ni lini barabara hiyo itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mhandisi Kasekenya amesema barabara hiyo ni muhimu kwa kuwa inaunganisha Mkoa wa Songwe (Ileje) na Mkoa wa Mbeya (Kyela), na kumhakikishia Mbunge huyo kuwa Serikali itazingatia maombi ya kuanza ujenzi kwa upande mwingine kulingana na ushauri wa Mhandisi Mshauri.
Vilevile, amemuelekeza Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mbeya kufika eneo la mradi huo kwa ajili ya ukaguzi na kuanza matengenezo ya barabara ya kiwango cha kawaida, ili kuhakikisha inapitika wakati wote.