MSONGAMANO WA MAGARI KUPUNGUA SONGWE, TANROADS YAJIPANGA NA MZANI MPYA IBOYA
Songwe, 06 Mei,2026
Kaimu Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe, Mhandisi Frederick Mande, amesema kuwa mkoa huo unaendelea kuboresha mifumo ya upimaji uzito wa magari kwa lengo la kuongeza ufanisi na kupunguza msongamano katika vituo vya mizani.
Ameeleza kuwa Mkoa wa Songwe, ambao unapakana na nchi za Zambia na Malawi, una jumla ya mizani miwili ya kudumu pamoja na mzani mmoja wa mkeka. Mizani ya kudumu ipo katika maeneo ya Mpemba na Ngangamo, huku mzani wa mkeka ukiwa Mpemba kwa ajili ya kuhudumia magari yanayotoka Tunduma kuelekea Mbeya.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mande, mzani wa kudumu wa Mpemba una mfumo wa weigh in motion unaowezesha kupima magari yakiwa katika mwendo, ambapo yale yanayobainika kuzidisha uzito hupelekwa kwenye mzani wa kawaida kwa ajili ya uhakiki zaidi.
Ameongeza kuwa magari yanayotoka Mbeya kuelekea Tunduma hupimwa katika mzani wa kudumu, huku yale yanayotoka Tunduma kuelekea Mbeya yakianza kupimwa katika mzani wa mkeka kabla ya kuthibitishwa katika mzani wa Mpemba.
Aidha, katika eneo la Ngangamo, mzani wa kudumu hutumika kupima magari yanayotoka na kuelekea mikoa ya Rukwa na Katavi pamoja na yale yanayosafiri kuelekea Tunduma.
Akizungumzia wastani wa magari yanayopimwa kwa siku, Mhandisi Mande amesema mzani wa Mpemba hupokea kati ya magari 700 hadi 1,200 kwa siku, huku mzani wa Ngangamo ukipokea kati ya magari 200 hadi 500.
Amebainisha kuwa mnamo Desemba 17, 2025, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alitoa maelekezo ya kufanyika kwa upembuzi yakinifu wa ujenzi wa mzani mpya katika eneo la Iboya, hatua inayolenga kupunguza msongamano wa magari katika mzani wa Mpemba.
Akifafanua kuhusu hatua hiyo, amesema mchakato wa manunuzi unaendelea kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa, na kwamba utekelezaji wa mradi huo ukikamilika unatarajiwa kuongeza ufanisi wa huduma za mizani na kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari katika eneo la Mpemba na maeneo ya jirani.
Mhandisi Mande ametoa wito kwa watumiaji wa barabara kutoa ushirikiano kwa TANROADS, akisisitiza kuwa changamoto zote zinazowasilishwa na madereva au wananchi hupokelewa, kufikishwa kwa mamlaka husika na kufanyiwa kazi kwa wakati.