WAZIRI MKUU AAGIZA TANROADS KUMPATA MKANDARASI BARABARA YA NYOLOLO - MTWANGO
Mufindi, 02 Mei, 2026
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameielekeza Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kuharakisha taratibu za kumpata mkandarasi atakayejenga barabara ya Nyololo–Mtwago yenye urefu wa kilometa 20 kwa kiwango cha lami katika Wilaya ya Mufindi, Mkoa wa Iringa, kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa maeneo hayo.
Dkt. Mwigulu ametoa maelekezo hayo, tarehe 02 Mei 2026, mkoani Iringa alipokuwa akizungumza na wananchi wa Mufindi, ambapo alisisitiza kuwa ujenzi wa barabara hiyo unapaswa kuanza mara moja kama ilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokutana na wananchi wa eneo hilo.
“Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya ujenzi wa barabara ya Nyololo–Mtwago, hivyo hakikisheni ndani ya wiki mbili mnapata mkandarasi wa kilometa hizi 20, na utekelezaji wake uanze ili kutimiza ahadi ya Mheshimiwa Rais wetu,” amesema Dkt. Mwigulu.
Mbali na hilo, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu ameelekeza barabara ya Mafinga–Mgololo yenye urefu wa kilometa 81 kuombewa malipo ya awali ili mkandarasi aanze kazi, akieleza kuwa barabara hiyo ni muhimu kwa shughuli za kiuchumi katika Mkoa wa Iringa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema Wizara imepokea maelekezo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi kwa haraka ili utekelezaji wake uanze mara moja.
Mkutano huo uliofanyika wilayani Mufindi ni sehemu ya mwendelezo wa ziara na mikutano ya Waziri Mkuu ya kukutana na wananchi, kusikiliza changamoto zao, na kutatua kero mbalimbali kwa wakati.