WAZIRI ULEGA ASEMA MRADI WA DARAJA LA MKWAJUNI UMEWAFAA WANANCHI, UTEKELEZAJI WAFIKIA 98%
Dar es salaam, 26 April,2026
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, amesema kuwa mradi wa daraja la Mkwajuni umeleta manufaa makubwa kwa wananchi na unaendelea vizuri chini ya mkandarasi mzawa, Kings Construction, kufuatia maelekezo ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha wakandarasi wazawa kushiriki katika miradi mikubwa ya maendeleo.
Amesema hayo Aprili 26, 2026, wakati wa ziara ya Waziri Mkuu aliyekagua miradi ya madaraja ya Mkwajuni na Kigogo.
Kwa mujibu wa Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Japherson Nnko, miradi hiyo ni sehemu ya mpango wa dharura wa CERC unaotekelezwa nchi nzima, ukiwa na jumla ya madaraja 81 yenye thamani ya Shilingi bilioni 553.9, yanayofadhiliwa na Benki ya Dunia.
Daraja la Mkwajuni lina urefu wa mita 20 pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa mita 660. Mradi wake umefikia asilimia 98, ukiwa na gharama ya Shilingi bilioni 11.6, ambapo tayari Shilingi bilioni 10.7 zimelipwa, na unatarajiwa kukamilika Mei 2026.
Kwa upande wa daraja la Kigogo, lina urefu wa mita 50 na barabara unganishi zenye urefu wa mita 625. Utekelezaji wake umefikia asilimia 89, ukiwa na gharama ya Shilingi bilioni 17.7, na unatarajiwa pia kukamilika Mei 2026.
Mhandisi Nnko amesema kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutaleta manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na kurahisisha usafiri, kupunguza gharama za usafirishaji, kuchochea shughuli za biashara, kuboresha huduma za usafiri wa mabasi yaendayo haraka (BRT) katika barabara ya Kawawa pamoja na kuongeza ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Jiji la Dar es Salaam