News

WAZIRI MKUU AKAGUA UJENZI WA MADARAJA YA MKWAJUNI NA KIGOGO, AIPONGEZA SERIKALI YA RAIS SAMIA KWA UBUNIFU NA UWEKEZAJI MKUBWA

WAZIRI MKUU AKAGUA UJENZI WA MADARAJA YA MKWAJUNI NA KIGOGO, AIPONGEZA SERIKALI YA RAIS SAMIA KWA UBUNIFU NA UWEKEZAJI MKUBWA

Dar es salaam, 26 April, 2026

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema hatua kubwa ya ujenzi wa madaraja nchini ni ushahidi wa ubunifu na uongozi madhubuti unaofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Ametoa kauli hiyo Aprili 26, 2026 mara baada ya kukagua madaraja ya Kigogo na Mkwajuni jijini Dar es Salaam.

Ameeleza kuwa madaraja ya Kigogo na Mkwajuni sasa yamejengwa juu ya usawa wa ardhi na kufikia kiwango cha ghorofa ya tatu, sawa na madaraja mapya ya Lindi na Mtwara.

Ametaja pia Daraja la Sitalike mkoani Katavi kuwa ni miongoni mwa madaraja ya aina hiyo. Kwa ujumla, madaraja 81 ya kiwango hicho yamejengwa nchini, hatua ambayo amesema haijawahi kutokea na imewezekana kutokana na uwezo wa Serikali kupata fedha kupitia ubunifu wa Rais Samia.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu, amesema Daraja la Jangwani litakuwa na urefu wa mita 390 sawa na viwanja vinne vya mpira na upana wa mita 42.8, unaoruhusu magari kupishana kwa urahisi. Urefu wake kutoka chini kwenda juu ni mita 15, hatua itakayomaliza historia ya mafuriko ya mara kwa mara eneo la Jangwani.

Ameongeza kuwa mradi huo unaenda sambamba na ujenzi wa madaraja mengine matatu yatakayotatua changamoto ya mafuriko jijini Dar es Salaam.

Aidha, amesema mradi mkubwa wa mifereji Boko Basihaya wenye thamani ya shilingi bilioni 57 uko katika hatua ya manunuzi, huku miradi ya Mzinga, Mpiji Chini na Ununio yenye thamani ya shilingi bilioni 46.5 ikiendelea kutekelezwa.

Kwa mujibu wa Waziri Ulega, miradi ya Kigogo na Mkwajuni iliyokaguliwa na Waziri Mkuu inagharimu shilingi bilioni 28.

Vilevile amesema kuwa, kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Serikali, wananchi wana wajibu wa kuendelea kuiunga mkono na kumuombea dua njema Rais Samia kwa juhudi zake za kuleta maendeleo nchini.