News

SERIKALI YAMWAGA BILIONI 5 MWANDEGE – MAEGESHO MAKUBWA YA MALORI YAJA KUBADILI UCHUMI

SERIKALI YAMWAGA BILIONI 5 MWANDEGE – MAEGESHO MAKUBWA YA MALORI YAJA KUBADILI UCHUMI

Pwani, 23 April, 2026

Serikali imetoa shilingi bilioni tano kwa ajili ya ujenzi wa eneo la kisasa la maegesho ya magari makubwa (malori) katika kata ya Mwandege, Wilaya ya Mkuranga, mkoa wa Pwani ikiwa ni hatua muhimu ya kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuchochea ukuaji wa uchumi wa ndani.

Akizungumza kuhusu mradi huo, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, amesisitiza kuwa Serikali ipo imara katika kutekeleza ahadi yake ya kujenga maegesho hayo, akibainisha kuwa mpango huo haujabadilika na utekelezaji wake unaendelea kama ulivyopangwa.

Amesema maegesho hayo yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi zaidi ya malori 360 kwa wakati mmoja, jambo litakalosaidia kupunguza msongamano na changamoto ya maegesho ya magari makubwa, huku yakiboresha mtiririko wa usafirishaji wa mizigo.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, mradi huo unatekelezwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ukiwa na lengo la kujenga miundombinu ya kisasa inayokidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya sekta ya usafirishaji.

Mbali na kuboresha huduma za usafirishaji, mradi huo unatarajiwa kufungua milango ya fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wakazi wa Mwandege na maeneo ya jirani.

Biashara ndogo ndogo kama za chakula, vinywaji na huduma nyingine za kila siku zinatarajiwa kushamiri, hivyo kuongeza kipato kwa wananchi.

“Mwandege inakwenda kuwa kitovu kipya cha biashara. Mama lishe, vijana na wananchi kwa ujumla watanufaika moja kwa moja na uwepo wa maegesho haya,” amesema Waziri Ulega.

Aidha, ameeleza kuwa mchakato wa kumpata mkandarasi uko katika hatua za mwisho, na maandalizi ya kuanza utekelezaji wa mradi yanaendelea kukamilishwa.

Waziri Ulega ametoa wito kwa wananchi, hususan vijana na wanawake, kujipanga kikamilifu ili kunufaika na fursa zitakazozaliwa na mradi huo, akisisitiza umuhimu wa kutumia nafasi hiyo kuboresha maisha yao na kuchangia maendeleo ya eneo hilo.