WAPENI USHIRIKIANO WAKANDARASI ILI MIRADI IKAMILIKE KWA WAKATI: WAZIRI ULEGA
Pwani, 21 April, 2026
Waziri wa Ujenzi Mh Abdallah Ulega leo Aprili 21, 2026 ameendelea na ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Mkuranga Mkoani Pwani ambapo amewahakikishia wakazi wa kijiji cha Kimanzichana kuwa serikali itaendelea kuleta fedha kutekeleza miradi ya kimkakati huku akiwataka kuiunga mkono.
Akiwahutubia wakazi wa Kijiji cha Kimanzichana ambako alifika kukagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Kimanzichana kupitia Mkamba hadi Msanga yenye urefu wa kilometa 43.83, amesema tayari serikali imeshatoa fedha zinazohitajika na kuongeza kuwa maadalizi ya utekelezaji wake yako katika hatua za mwisho.
" Ndugu wananchi, niwahakikishie serikali yenu inayoongozwa na Rais wetu mpedwa Dkt Samia Suluhu Hassan iko kazini usiku na mchana ili kuwawekea mazingira rafiki ya kutekeleza shughuli zenu za maendeleo, hapa uthibitisho ulio wazi unaoonyesha anawajali ni kitendo cha kuwaletea fedha nyingi za mradi huu zaidi ya shilingi bilioni 2" alisisitiza Waziri Ulega.
Aidha Waziri Ulega amewaahidi wakazi wa Kimanzichana kuwa utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuendelea hivi karibuni mara baada ya kipindi cha masika kumalizika huku akimuagiza Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) kuhakikisha anasimamia kwa karibu utekelezaji wake.
Pia Waziri Ulega ameutumia mkutano huo kumwagiza meneja wa mradi huo kutoa kipaumbele cha ajira za muda kwa wazawa wa eneo hilo hatua ambayo amesema itawasaidia kujiongezea kipato na kuondoa manung'uniko miongoni mwa wananchi.
Kwa upande wao wakazi wa Kimanzichana waliofurika kwa wingi katika mkutano huo wa hadhara kijijini hapo wameishukuru serikali kwa kuwapelekea fedha za mradi na kusisitiza kuwa kukamilika kwake kutasaidia kutatua changamoto ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa zao yakiwemo mazao ya kilimo na biashara.