News

WAZIRI ULEGA ATOA SIKU 14 KWA TANROADS KUMPATA MKANDARASI BARABARA YA KISARAWE - MANEROMANGO, ASISITIZA UTEKELEZAJI WA HARAKA NA KWA KUZINGATIA SHERIA

WAZIRI ULEGA ATOA SIKU 14 KWA TANROADS KUMPATA MKANDARASI BARABARA YA KISARAWE - MANEROMANGO, ASISITIZA UTEKELEZAJI WA HARAKA NA KWA KUZINGATIA SHERIA

Pwani, 21 April,2026

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, ameagiza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kukamilisha mchakato wa kumpata mkandarasi wa ujenzi wa barabara ya Kisarawe hadi Maneromango, wilayani Kisarawe, ndani ya wiki mbili, akisisitiza umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wa mradi huo bila kukiuka taratibu za kisheria.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Masaki, wilayani Kisarawe mkoani Pwani, Mhe. Ulega amesema anatarajia ndani ya kipindi hicho kupatikana kwa mkandarasi atakayetekeleza mradi huo, ili aweze kurejea eneo hilo kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa ujenzi, akishirikiana na mbunge pamoja na madiwani wa eneo husika.

“Wana Masaki, leo kazi yangu ni moja tu - kuiagiza TANROADS kukamilisha taratibu zote za kitaalamu ili ujenzi uanze. Ni matumaini yangu mmeshakamilisha taratibu zenu za ndani, hivyo ndani ya wiki mbili nahitaji kufahamu ni mkandarasi gani amekidhi vigezo ili aingie site na kuanza kazi,” alisisitiza Mhe. Ulega.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wananufaika na huduma zote muhimu za kijamii zikiwemo elimu, afya, miundombinu na kilimo, hatua itakayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi.

Aidha, amebainisha kuwa Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo ikiwemo ya barabara ili kuhakikisha wananchi wanapata manufaa ya moja kwa moja.

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega amerejea maelekezo ya Rais yanayotaka barabara zote mpya ziwekwe taa za barabarani ili kuongeza usalama na kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika saa zote.

Ameongeza kuwa uwekaji wa taa katika maeneo ya miji, ikiwemo Masaki wilayani Kisarawe, utasaidia kuchochea biashara ndogondogo na ajira, hususan kwa mama lishe, waendesha bodaboda na wafanyabiashara wengine.

Sambamba na hilo, amewaagiza Mameneja wa TANROADS na TARURA Mkoa wa Pwani kuweka utaratibu madhubuti wa utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa kuzingatia sheria na taratibu, akisisitiza kuwa uwajibikaji wao utaongeza imani ya wananchi kwa Serikali.

Pia amewataka wataalamu kuweka mikakati endelevu ya kuhakikisha barabara zinajengwa kwa ubora na kuwekewa taa ili kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika hata nyakati za usiku.

Aidha, ametoa maagizo ya dharura kushughulikia barabara iliyokatika katika eneo la Vikumburu, akitaka wahusika kurejesha mawasiliano haraka na kuweka kambi ya muda ili kazi hiyo ifanyike mchana na usiku hadi itakapokamilika.

Akijibu ombi la Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Dkt. Suleiman Jaffo, kuhusu uharibifu wa barabara ya Dondwe–Lukwali hadi Njia Nne, Waziri Ulega ameagiza wataalamu kufika mara moja eneo hilo na kuanza kazi za matengenezo bila kuchelewa.

Vilevile, amewaelekeza Mameneja wa TANROADS na TARURA Mkoa wa Pwani kuandaa mpango kazi maalum wa ukarabati wa barabara zote zilizoathiriwa na mvua ili ziweze kurejeshwa katika hali nzuri.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, Dkt. Suleiman Jaffo, amesema hali ya miundombinu imekuwa changamoto kubwa, akieleza kuwa baadhi ya mabasi yamelazimika kusimama kwa muda mrefu kutokana na ubovu wa barabara.

Miongoni mwa wananchi, msanii na mkazi wa Kisarawe, Madebe Lidai, ameeleza kuridhishwa kwake na mradi huo, akisema utaleta mageuzi makubwa katika usafiri na uchumi wa eneo hilo.

“Sisi tunashukuru kwa hii barabara yenye urefu wa kilometa 34.5 kutoka hapa Sungwi hadi Maneromango itatusaidia vyombo vya usafiri kuwa salama na kufika kwa haraka zaidi,” alisema Madebe Lidai.

Wananchi wengine wameeleza kuwa barabara hiyo inaunganisha maeneo muhimu yakiwemo Bwawa la Mwalimu Nyerere, Hifadhi ya Selous na Mloka wilayani Rufiji, hivyo itachochea shughuli za biashara na uwekezaji katika ukanda huo.Wamesema kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha biashara, upatikanaji wa huduma za kijamii na kufungua fursa mpya za maendeleo kwa wananchi wa Kisarawe na maeneo jirani.

Mradi huo wa ujenzi wa barabara wenye urefu wa kilometa 34.5 unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya viwanda katika Wilaya ya Kisarawe.