MTANDAO WA BARABARA ZA TANZANIA NI KILOMETA 16,000, ZILE TAKWIMU ZILIKUWA ZA KUTUDOGOSHA TU — ULEGA
Dar es salaam, 20 April,2026
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, amesema Tanzania ina mtandao mkubwa wa barabara za lami unaofikia kilometa 16,000, akibainisha kuwa takwimu zilizowahi kutolewa na mmoja wa viongozi kutoka nchi jirani kuhusu ukubwa wa mtandao huo “zilikuwa za kutudogosha” na hazikuakisi maendeleo halisi ya sekta ya miundombinu nchini.
Ametoa kauli hiyo Aprili 20, 2026 wakati akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba wa uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi, iliyofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Ulega alisema utekelezaji wa mradi huo mkubwa unaoongozwa na Serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, utaandika historia mpya ya maendeleo na kuimarisha ustahimilivu wa miundombinu katika Jiji la Dar es Salaam.
Waziri huyo wa Ujenzi amefafanua kuwa, Tanzania ni miongoni mwa nchi mbili za Afrika Mashariki zilizo katika kundi la uchumi wa kati wa chini, akisema hadhi hiyo inaendana na kasi ya uwekezaji mkubwa katika sekta ya barabara.
Kwa mujibu wa Ulega, mtandao wa barabara za serikali zilizorekodiwa katika gazeti la serikali unafikia kilometa 182,000, huku barabara nyingi zaidi zikiendelea kufunguliwa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Vilevile ametoa wito kwa TARURA kuwasilisha barabara zote mpya ili ziingizwe rasmi kwenye gazeti la serikali ili kuifanya nchi kuwa na takwimu Sahihi ya mtandao wa barabara zote nchini.
Mhe. Ulega amesema baadhi ya nchi jirani zina takribani kilometa 6,100 za barabara za lami, na kwamba ukijumlisha na za Tanzania, mtandao huo unafikia zaidi ya kilometa 22,000, hivyo madai kwamba Afrika Mashariki haiwezi kufikia kilometa 20,000 “hayana msingi”.
Aidha, amebainisha kuwa barabara zenye urefu wa kilometa 5,100 zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi, huku miradi mingine yenye jumla ya kilometa 3,700 ikiwa tayari imeshasajiliwa na kupangiwa wakandarasi.
Ulega amesema wakati wa uhuru Tanzania ilirithi chini ya kilometa 600 za barabara za lami, na kwa mba zaidi ya kilometa 15,000 zilizopo sasa na Watanzania ndani ya Tanzania huru, tofauti na baadhi ya nchi jirani ambazo zilipokea mtandao mkubwa wa barabara kutoka kwa wakoloni.
Vilevile amesisitiza kuwa Tanzania imejengwa na itaendelea kujengwa na Watanzania wenyewe, huku Serikali ikiendelea kuwekeza katika miradi mikubwa ya kimkakati ili kuimarisha uchumi na kuboresha huduma kwa wananchi.