News

MIRADI YA BARABARA ZA NJIA NNE NA UWANJA WA AFCON KUIBADILISHA ARUSHA - WAZIRI MKUU

MIRADI YA BARABARA ZA NJIA NNE NA UWANJA WA AFCON KUIBADILISHA ARUSHA – WAZIRI MKUU Arusha, 17 April, 2026 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema miradi mikubwa ya barabara na ujenzi wa Uwanja wa mpira wa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) itaibadilisha kwa kiasi kikubwa sura ya Jiji la Arusha na kulifanya kuwa kitovu cha kimataifa cha utalii na biashara. Akizungumza Aprili 17, 2026 katika mkutano wa hadhara Kona ya Mbauda, Waziri Mkuu alieleza kuwa mafanikio ya miradi hiyo yametokana na uongozi thabiti wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amewezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo mikubwa ya kimkakati. Alisema miradi hiyo inajumuisha barabara za njia nne, taa za kisasa za barabarani, pamoja na miundombinu ya biashara ikiwemo stendi na masoko ya kisasa, itakayolifanya Arusha kuwa na mwonekano wa kisasa na wa kipekee. Serikali tayari imetoa shilingi Bilioni 10.2 kwa ajili ya fidia, huku mkandarasi akishalipwa malipo ya awali na utekelezaji wa ujenzi ukiendelea. Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega, alimshukuru Rais kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi hiyo, akisisitiza kuwa uwekaji wa taa za kisasa utaimarisha usalama, ambapo kila kilometa moja itawekewa taa 40, na barabara ya Arusha Bypass itawekwa zaidi ya taa 1,600. Aidha, barabara ya Kilombero - Kisongo (Km 9) itawekewa taa 360 na kujengewa mitaro mikubwa itakayopitisha maji ili kudhibiti mafuriko. Mbunge wa Arusha Mjini, Mhe. Paul Makonda, alisema miradi hiyo imeleta matumaini mapya kwa wananchi, akibainisha kuwa ujenzi wa barabara za kisasa utarahisisha usafiri, usafirishaji, kuimarisha usalama na kuchochea shughuli za kiuchumi. Awali, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, alisema mkandarasi wa barabara ya Mbauda–Losinyai na Tanganyika Packers alianza kazi Aprili 10, 2026, na mradi unatarajiwa kukamilika Aprili 9, 2029, huku kipande cha Km 13 (Mbauda–Bondeni City) kikitarajiwa kukamilika kabla ya mashindano ya AFCON 2027. Aliongeza kuwa Km 7 zitajengwa kwa njia nne na Km 63 kwa njia mbili chini ya mkandarasi China Civil Engineering Construction Company Corporation, aliyelipwa awali shilingi Bilioni 17.6. Pia, mradi wa Kilombero–Kisongo (Km 9.1) umetangazwa zabuni Aprili 15, 2026 na kufunguliwa Aprili 30, 2026. Serikali imejipanga kuhakikisha miradi hii inakamilika kwa wakati, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mashindano ya mpira wa miguu ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 na mwanzo wa mageuzi makubwa ya miundombinu yatakayoiweka Arusha katika ramani ya miji ya kisasa duniani.