TANROADS YAIMARISHA USALAMA BARABARANI KUPITIA UBORESHAJI WA ALAMA ZA ZEBRA DAR ES SALAAM
Dar es salaam, 15 April, 2026
TANROADS imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha usalama wa miundombinu ya barabara kwa kufanya ukarabati na upakaji rangi mpya kwenye alama mbalimbali za barabarani, hususan alama za watembea kwa miguu (zebra crossing), kwa lengo la kupunguza ajali.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha barabara zinabaki katika hali nzuri na rafiki kwa watumiaji wote, wakiwemo madereva na watembea kwa miguu ambao ni miongoni mwa makundi hatarishi.
Zoezi la kuboresha alama hizo linaendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, likiwemo eneo la makutano ya barabara karibu na ITV, pande zote mbili, pamoja na kituo cha mabasi ya daladala cha ITV Mwenge.
Katika utekelezaji huo, alama zilizofifia au kufutika zinapakwa rangi upya ili kuongeza uonekano wake, hatua inayowasaidia madereva na watembea kwa miguu kuzitambua kwa urahisi na hivyo kupunguza ajali zisizo za lazima.
Aidha, maboresho hayo yameongeza mwonekano wa alama hizo hususan nyakati za usiku au wakati wa mvua, hali inayochangia madereva kuchukua tahadhari mapema wanapokaribia maeneo ya kuvuka barabara.
Kwa mujibu wa TANROADS, zoezi hilo ni endelevu na litaendelea kufanyika katika maeneo yote ambayo alama za barabarani zimefifia au hazionekani kwa urahisi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha barabara zinakuwa salama na zenye viwango vinavyokubalika.
Wakala ya Barabara pia imewahimiza wananchi kuzingatia alama za barabarani na kufuata sheria ili kulinda usalama wao na wa watumiaji wengine wa barabara.