News

TANROADS YAZALISHA AJIRA ZAIDI YA 500 KUPITIA MRADI WA UJENZI WA BARABARA NTYUKA–MVUMI–KIKOMBO

TANROADS YAZALISHA AJIRA ZAIDI YA 500 KUPITIA MRADI WA UJENZI WA BARABARA NTYUKA–MVUMI–KIKOMBO

Dodoma, 12 April, 2026

Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, amefanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa barabara ya lami ya Ntyuka–Mvumi–Kikombo yenye urefu wa kilomita 76, pamoja na kipande cha barabara ya Chololo–Mapinduzi (Makao Makuu ya TPDF) chenye urefu wa kilomita 5, katika Jimbo la Mvumi, Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma.

Mradi huo unaotekelezwa na TANROADS kwa ufadhili wa asilimia 100 kutoka Serikali ya Tanzania, unalenga kuimarisha mtandao wa barabara, kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa, pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika eneo hilo, hususan kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu kama Hospitali ya Mvumi Mission.

Ujenzi wa mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili kuu:

Awamu ya kwanza yenye urefu wa kilomita 25 (Ntyuka–Mvumi–Makulu na Kikombo–Chololo–Mapinduzi) imefikia asilimia 80.9 ya utekelezaji. Awamu hii inatekelezwa na Mkandarasi M/s China Henan International Corporation Company Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 38.199.

Awamu ya pili yenye urefu wa kilomita 53 (Ntyuka–Mvumi Hospitali–Kikombo) imeanza kutekelezwa na Mkandarasi China First Highway Engineering Co. Ltd, na hadi sasa imefikia asilimia 5.2 ya utekelezaji, ikiwa na thamani ya shilingi bilioni 98.488.

Mradi huo pia umekuwa chanzo cha ajira kwa wananchi, ambapo zaidi ya Watanzania 500 wamehusishwa moja kwa moja katika hatua mbalimbali za ujenzi.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi, Mhandisi Jefferson Nko alieleza maendeleo yaliyofikiwa, changamoto zinazoikabili kazi hiyo pamoja na mikakati iliyowekwa kuhakikisha inakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.

Akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo, Waziri Mkuu alisema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha miundombinu kama msingi wa ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.

Alisisitiza kuwa barabara hiyo ni muhimu kiuchumi kwa kuwa inapita katika maeneo yenye uzalishaji, hivyo kukamilika kwake kutafungua fursa zaidi za biashara na huduma kwa wananchi.

Aidha, aliwataka wakandarasi kuongeza kasi ya utekelezaji huku wakizingatia ubora na muda wa mkataba ili mradi ukamilike kwa wakati uliopangwa.