DARAJA LA KATUMBA LAFUNGUA FURSA ZA KIUCHUMI MIKOA YA RUKWA NA KATAVI, SASA LINAPITIKA MAJIRA YOTE YA MWAKA
Katavi, 12 April,2026
Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha ujenzi wa Daraja la Katumba lenye urefu wa mita 60 katika eneo la Mirumba , kwa gharama ya shilingi bilioni 6.399, hatua inayotarajiwa kuboresha mawasiliano na kukuza uchumi kati ya mikoa ya Katavi na Rukwa.
Akizungumza kuhusu ujenzi wake, Kaimu Meneja TANROADS Mkoa wa Katavi, Mhandisi Aumsuri Jacob, amesema ujenzi wa daraja hilo ulianza Novemba 2024 na kukamilika Februari 2026.
Ameongeza kwa kusema kuwa, daraja la Katumba ni kiunganishi muhimu kati ya mikoa Katavi na Rukwa, likirahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa na hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi.
“Daraja hili sasa linapitika mwaka mzima, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo eneo hili lilikuwa linakumbwa na mafuriko ya mara kwa mara yaliyosababisha usumbufu mkubwa wa usafiri,” alisema Mhandisi Jacob.
Akifafanua zaidi amesema, mwaka 2023 daraja la awali lilikatika kabisa na kusababisha barabara kufungwa kwa muda, hali iliyoilazimu serikali kujenga daraja la muda la chuma kabla ya kuanza ujenzi wa daraja la kudumu la zege.
Mbali na kuboresha mawasiliano kati ya Katavi na Rukwa, daraja hilo pia limefungua njia mbadala ya usafiri kuelekea Tabora.
Kwa sasa msafiri anaweza kutoka Sumbawanga bila kupitia Panda, akapitia daraja hilo hadi Majimoto, kisha Mlele na kuendelea na safari kuelekea Tabora.
Kwa upande wa ajira, mradi huo umetoa nafasi 51 za ajira za kudumu kwa wananchi, hatua iliyochangia kuongeza kipato katika jamii inayozunguka eneo la mradi.
Ujenzi wa daraja hilo umetekelezwa na kampuni za wazawa, Safari Business Contractors kwa kushirikiana na Mbuya Building Contractors, zote zenye makao yake Sumbawanga.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Mhandisi Vides Sanga kutoka Safari General Business Contractors Co. Ltd amesema, kampuni yake inajivunia kuaminiwa na serikali kutekeleza mradi huo mkubwa.
Amesema serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikiendelea kuwapa kipaumbele wakandarasi wazawa, hatua inayochochea ukuaji wa uwezo wao kiteknolojia na kiuchumi.
“Kupitia usimamizi wa TANROADS katika miradi kama hii, tumepata uzoefu na kuimarisha uwezo wetu. Tunaamini tunaweza kuaminiwa zaidi kutekeleza miradi mikubwa ya kitaifa,” alisema Mhandisi Sanga.