News

ULEGA AIPONGEZA TANROADS KWA UTEKELEZAJI WA MIRADI 81 YA DHARURA

ULEGA AIPONGEZA TANROADS KWA UTEKELEZAJI WA MIRADI 81 YA DHARURA 

Morogoro, 10 April, 2026

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameipongeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) na kuridhika kwa kazi kubwa ya kusimamia utekelezaji wa miradi 81 ya dharura iliyofanyika kwa ufanisi katika mikoa mbalimbali nchini.

Miradi hiyo iliyojumuisha ujenzi wa madaraja na makalvati kupitia mpango wa Contingent Emergency Response Component (CERC), unaolenga kushughulikia majanga ya dharura katika miundombinu, imeelezwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha miundombinu na kupunguza athari za mafuriko hususan wakati wa mvua kubwa.

Akizungumza mkoani Morogoro wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 21 wa Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS, Waziri Ulega amesema miradi hiyo imekamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika, huku ikitekelezwa na wakandarasi wazawa jambo linalodhihirisha kuimarika kwa uwezo wa ndani wa kitaalamu.

Aidha, amempongeza Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha zilizochangia utekelezaji wa miradi hiyo, akibainisha kuwa uwekezaji huo tayari unaonyesha matokeo chanya.

Ameongeza kuwa licha ya mvua zinazoendelea kunyesha nchini, athari zake zimepungua ikilinganishwa na miaka iliyopita, hali inayochangiwa na uwepo wa miundombinu bora iliyojengwa.

“Utekelezaji wa miradi hii unaonyesha uwezo mkubwa wa wataalamu wa TANROADS katika kukabiliana na changamoto za miundombinu, hususan zinazotokana na mafuriko,” amesema Ulega, huku akihimiza tathmini zaidi ili kubaini maeneo mengine yanayohitaji maboresho.

Katika hatua nyingine, Waziri Ulega amewasisitiza watumishi wa TANROADS kuendelea kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na kuzingatia nidhamu, huku wakilinda misingi ya taasisi hiyo ili kuendelea kuboresha miundombinu ya nchi.

Pia, ameelekeza umuhimu wa kufanya matengenezo ya barabara na madaraja kwa wakati ili kuepusha usumbufu kwa wananchi, na pamoja na kutekeleza mpango wa upandaji miti ya kivuli na matunda takribani 1,000 kwa kila mkoa na kusimika taa za barabarani.