SERIKALI YAENDELEA KUJENGA BARABARA ZA USALAMA MIPAKANI KUIMARISHA ULINZI
Dodoma, 10 April, 2026
Serikali imesema inaendelea kujenga barabara za usalama mipakani kwa kiwango cha changarawe, ili kuhakikisha mipaka ya nchi inakuwa salama na kuwezesha vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha doria.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, leo Aprili 10, 2026, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Happiness Daniel Ngwando, aliyeuliza kuhusu mpango wa Serikali wa kuboresha barabara za mipakani ili kusaidia shughuli za ulinzi na usalama.
Akijibu swali hilo, Mhandisi Kasekenya alieleza kuwa barabara hizo ni muhimu kwa kuwa zinapita kando ya mipaka ya nchi na kusaidia vyombo vya usalama kufanya doria kwa ufanisi zaidi.
Amefafanua kuwa hadi sasa Serikali, kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), imejenga jumla ya kilometa 1,759 za barabara za mipakani kwa kiwango cha changarawe katika mikoa mbalimbali ya mipakani.
Aidha, ujenzi wa sehemu zilizobaki unaendelea kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
“Kwa kutambua umuhimu wa barabara hizi, Serikali inaendelea kuzijenga kwa kiwango cha changarawe ili ziweze kutumika wakati wote na vyombo vya usalama kufanya doria mipakani,” amesema Mhandisi Kasekenya.
Kuhusu barabara ya Mtwara – Pachani – Tunduru (km 300), Mhandisi Kasekenya amesema kuwa usanifu wake tayari umekamilika, na kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami.