News

MIRADI YA DHARURA YA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 17 YATEKELEZWA MKOA WA KATAVI

MIRADI YA DHARURA YA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 17 YATEKELEZWA MKOA WA KATAVI

08 April, 2026

Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), imetekeleza miradi mitatu ya dharura yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 17 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia katika Mkoa wa Katavi, ikiwa ni jitihada za kuboresha miundombinu ya barabara na kuondoa changamoto za usafiri zilizokuwa zikisababishwa na mvua kubwa.

Hayo yameelezwa na Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Katavi, Mhandisi Aumsuri Jacob Temu, ambaye amesema miradi hiyo ilitekelezwa kupitia mpango wa Contingent Emergency Response Component (CERC), unaolenga kushughulikia majanga ya dharura katika miundombinu.

Kwa mujibu wa Mhandisi Jacob, sehemu ya miradi hiyo imehusisha ujenzi wa madaraja matatu katika mito mikuu mkoani humo, ambapo daraja la Mto Katuma lililopo eneo la Sitalike liligharimu shilingi bilioni 9.16.

Amesema daraja hilo lenye urefu wa mita 55 lilijengwa kufuatia athari kubwa zilizotokea mwaka 2024 baada ya mvua kubwa kusababisha barabara kuu inayoelekea Sumbawanga kufungwa kwa siku 11, hali iliyokatiza mawasiliano na shughuli za kiuchumi.

“Serikali iliona umuhimu wa kuchukua hatua za haraka kwa kutoa fedha za ujenzi wa daraja hili ili kuondoa changamoto hiyo,” alisema Mhandisi Jacob.

Ameongeza kuwa ujenzi wa daraja hilo ulianza Novemba 2024 na kukamilika Januari 2026, na sasa umewezesha barabara hiyo kupitika kwa urahisi katika kipindi chote cha mwaka.

Amefafanua kuwa daraja hilo ni sehemu ya barabara kuu inayounganisha Tunduma, Sumbawanga, Mpanda, Kigoma hadi Nyakanazi, ambayo pia hutumiwa na magari ya mizigo na abiria kutoka nchi za Afrika Kusini, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini.

Kufuatia kukamilika kwa mradi huo, Mhandisi Jacob amesema, daraja hilo limeimarisha usafiri na biashara za kikanda, sambamba na kupunguza adha kwa wananchi waliokuwa wakikumbwa na changamoto za usafiri wakati wa mvua.

Mradi huo umetekelezwa na mkandarasi mzawa wa Sumbawanga, Kampuni ya Mselemu Building Contractors, ambaye alikamilisha kazi hiyo kwa wakati na daraja hilo linaendelea kutumika bila matatizo.