MATUMIZI YA AWALI YA BARABARA YA MZUNGUKO WA NJE DODOMA (DODOMA OUTER RING ROAD) YAANZA KUPUNGUZA MSONGAMANO
Dodoma, 07 April, 2026
Matumizi ya awali ya barabara ya Mzunguko wa Nje ya Jiji la Dodoma (Dodoma Outer Ring Road) yameanza, hatua inayochangia kupungua kwa kiasi kikubwa cha msongamano wa magari ndani ya jiji, hususan yale makubwa ya mizigo.
Akizungumza katika eneo la mradi, Mkuu wa Mradi huo, Mhandisi Morice Mlay, amesema barabara hiyo tayari imeanza kutumika kwa kiwango fulani licha ya kutokukamilika rasmi, ambapo matumizi yameonekana zaidi kuanzia eneo la mzunguko wa Ihumwa (sheli ya jeshi) kuelekea Nala.
Amesema mradi huo una urefu wa jumla ya kilometa 104, huku sehemu ya kwanza yenye kilometa 52 (Lot 1) ikiwa chini ya usimamizi wake ambapo hadi sasa umefikia zaidi ya asilimia 92 ya utekelezaji.
Kwa mujibu wa Mhandisi Mlay, mradi unasimamiwa na kampuni ya Ushauri ya Interconsult, huku ujenzi ukifanywa na kampuni ya China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC).
Mhandisi Mlay amesema kuwa mradi huo unaunganisha barabara kuu zinazoelekea Arusha, Singida na Iringa, hivyo kuwa na mchango mkubwa katika kukuza shughuli za kiuchumi ndani na nje ya Jiji la Dodoma.
Barabara hiyo inatarajiwa kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya uchumi na usafirishaji, huku ikirahisisha mtiririko wa magari na kupunguza muda wa safari kwa watumiaji wake.
Amesisitiza kuwa barabara hiyo imeanza kuleta nafuu ya msongamano wa magari, hasa malori ambayo hapo awali yalikuwa yakipita katikati ya jiji, na sasa yanatumia njia hiyo ya mzunguko.
“Hii ni barabara ya kimkakati ambayo itaendelea kuwa mkombozi kwa kupunguza msongamano na kurahisisha usafirishaji wa mizigo,” amesema Mhandisi Mlay.
Hatahivyo, ameeleza kuwa kazi zinazoendelea kwa sasa ni pamoja na ujenzi wa njia za watembea kwa miguu, uwekaji wa mawe ya pembeni (curbestone) na mifereji ya maji ya mvua, huku pia maandalizi ya barabara za huduma (service roads) yakiendelea ili kurahisisha matumizi kwa wakazi wa maeneo jirani.
Barabara hiyo imejengwa kwa kiwango cha njia mbili kila upande (dual carriageway), zikitenganishwa na tuta la katikati, ikiwa ni sehemu ya miundombinu ya kisasa inayolenga kuongeza ufanisi wa usafiri na usafirishaji.
Katika hatua nyingine, ujenzi wa miundombinu muhimu unaendelea, ikiwemo daraja linalopita juu ya reli pamoja na vikutashoto (roundabouts) katika maeneo ya Nala, Veyula, Mahomanyika na Ihumwa.
Aidha, kazi za uboreshaji wa mandhari zinaendelea kwa kupanda miti na maua katika tuta la katikati na kwenye maeneo ya mizunguko ili kuongeza mvuto wa barabara hiyo.
Kuhusu gharama, Mhandisi Mlay amesema ujenzi wa barabara hiyo unagharimu takriban shilingi bilioni 100, huku gharama za mshauri zikiwa shilingi bilioni 4.5.