News

TANROADS YASHIRIKI MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI LA WIZARA YA UJENZI

TANROADS YASHIRIKI MKUTANO WA BARAZA LA WAFANYAKAZI LA WIZARA YA UJENZI

Dodoma, 31 Machi, 2026

Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Japherson Nnko, ameshiriki Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi la Wizara ya Ujenzi lililofanyika tarehe 30 - 31 Machi, 2026 kwenye ukumbi wa Mabele, Jijini Dodoma.

Mbali na Mhandisi Nnko, wengine walioshiriki kwenye mkutano huo wa baraza wakiwa ni wajumbe ni pamoja na Katibu wa Baraza la Wafanyakazi (TANROADS), Bi. Fatma Matimba na Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi (TAMICO), Mhandisi Nchama Wambura.

Katika ufunguzi wa mkutano huo Waziri Abdallah Ulega aliyekuwa mgeni rasmi, alisisitiza umuhimu wa taasisi zilizopo chini ya Wizara hiyo, kuwa na nidhamu, uwajibikaji na ufanisi.

Pia ameelekeza kila taasisi kuwasilisha kwa wakati taarifa za utendaji wa bodi zao ili kuiwezesha Wizara kupanga na kutekeleza mipango yake kwa uhakika na kuleta tija.

"Taasisi zote hapa za TEMESA, TBA, TANROADS, ERB, CRB, NCC,AQRB,RFB, ICoT na Vikosi vya ujenzi fanyeni kazi kwa weledi, bidii, maarifa kuongeza kasi ya utekelezaji na kuepuka rushwa ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ikiwemo kupata tija", alisisitiza Waziri Ulega.

Katika hatua nyingine Waziri Ulega ameelekeza kwa TANROADS, kuhakikisha wanasimamia vyema miradi ya miundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege, ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Katika ufungaji wa mkutano huo wa baraza Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewataka watumishi kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na weledi, wakihakikisha wanaweka mbele maono ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuleta tabasamu kwa wananchi kutokana na huduma bora wanayowapatia.

Pia amewasihi kufanya mazoezi ili kujiepusha na changamoto za magonjwa nyemelezi pamoja na afya ya akili na msongo wa mawazo, pia kutafuta vyanzo sahihi vya mapato na kujiepusha na vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya ofisi, ili kufikia malengo ya Serikali na kuleta tija kwa wananchi.

Halikadhalika, Mhandisi Kasekenya amesisitiza umuhimu wa watumishi kuwa na msukumo wa kufanya kazi ili kuongeza ujuzi na maarifa ambapo vinapelekea kufanya kazi kwa uhuru na kujituma.