TANROADS Yaandika Historia Mpya kwenye Viwanja vya Ndege
Dodoma, 30 machi,2026
Serikali kupitia TANROADS (Wakala wa Barabara Tanzania) imepata mafanikio makubwa katika ujenzi wa miundombinu ya viwanja vya ndege tangu ilipopewa jukumu hilo mwaka 2017.
Hadi sasa, jumla ya viwanja vya ndege 7 vimekamilika, vikiwemo Julius Nyerere International Airport (Terminal III), Mwanza, Mtwara, Songea, Songwe na Geita, hatua inayoboreshwa kwa kiwango kikubwa huduma za usafiri wa anga nchini.
Kwa upande wa miradi inayoendelea, viwanja vya ndege 8 vinaendelea kujengwa, ambapo baadhi ya miradi inaonesha uwekezaji mkubwa wa Serikali. Mfano, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato (Dodoma) unatekelezwa kwa gharama inayokadiriwa kufikia zaidi ya Shilingi bilioni 360–370, ukiwa katika hatua za mwisho za ujenzi na ukigawanyika katika vipengele vikuu viwili vya takriban Shilingi bilioni 165.6 (miundombinu ya kurukia ndege) na Shilingi bilioni 194.4 (majengo na huduma muhimu).
Miradi mingine kama Musoma, Shinyanga, Sumbawanga na Kigoma pia inaendelea kwa gharama za mabilioni ya shilingi, ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Uwekezaji huu mkubwa unaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha uchumi wa taifa, kukuza utalii, na kurahisisha usafiri wa anga, huku TANROADS ikiendelea kusimamia miradi hii kwa viwango vya ubora na ufanisi wa hali ya juu.