BRT AWAMU YA TATU YAVUTIA BUNGE: UWEKEZAJI WA SERIKALI WAPONGEZWA, MATUMAINI MAPYA KWA USAFIRI DAR
Dar es Salaam, 24 Machi, 2026
Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Awamu ya Tatu umeendelea kuonesha mafanikio makubwa baada ya kuvutia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), iliyofanya ziara maalum jijini Dar es Salaam na kuridhishwa na kasi na ubora wa utekelezaji wake.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Masanja Kadogosa, alisema wabunge wamevutiwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akibainisha kuwa mradi huo ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya kuboresha miundombinu ya usafiri wa umma nchini.
Alieleza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutakuwa suluhisho muhimu kwa changamoto ya msongamano wa magari jijini Dar es Salaam, huku ukitarajiwa kuongeza ufanisi, urahisi na upatikanaji wa huduma bora za usafiri kwa wananchi.
“Thamani ya fedha za Serikali inaonekana wazi kupitia ubora wa kazi zilizotekelezwa,” alisisitiza Kadogosa, akieleza kuridhishwa kwa kamati hiyo na viwango vya juu vya miundombinu iliyojengwa.
Aidha, aliipongeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa usimamizi madhubuti wa ujenzi wa miundombinu hiyo pamoja na DART kwa jukumu lake la kuratibu mfumo wa usafiri wa mabasi yaendayo haraka, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ndio chachu ya mafanikio ya mradi.
Kadogosa alibainisha kuwa Kamati itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo hadi kukamilika kwake ifikapo Aprili 30, 2026, huku akihimiza maandalizi ya kuanza kwa huduma mara moja baada ya kukamilika kwa ujenzi.
Kwa upande mwingine, alitoa wito kwa wananchi, hususan wakazi wa Dar es Salaam, kushiriki kikamilifu katika kulinda na kutunza miundombinu hiyo ili idumu na kuwanufaisha kwa muda mrefu.
Pia aliwataka TANROADS na DART kuendelea na matengenezo ya mara kwa mara ili kuhakikisha huduma zinaendelea kuwa bora na endelevu.
Mradi wa BRT Awamu ya Tatu unaendelea kuwa alama ya mageuzi ya usafiri wa umma nchini - ukifungua ukurasa mpya wa usafiri wa kisasa, salama na wenye ufanisi kwa wakazi wa Dar es Salaam.