News

SERIKALI YATOA TRILIONI 1.319 KUIMARISHA MIUNDOMBINU, ULEGA AELEZA MAFANIKIO SEKTA YA UJENZI

SERIKALI YATOA TRILIONI 1.319 KUIMARISHA MIUNDOMBINU, ULEGA AELEZA MAFANIKIO SEKTA YA UJENZI

Dodoma, 23 Machi, 2026

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuwa Serikali imeendelea kupiga hatua katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambapo hadi kufikia Machi 2026 jumla ya shilingi trilioni 1.319 tayari zimetolewa kwa ajili ya miradi iliyoidhinishwa katika mwaka wa fedha 2025/2026.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na makadirio ya mwaka 2026/2027 kwa fungu 98 la Wizara ya Ujenzi, leo Machi 23, 2026 Mkoani Dodoma, Ulega alieleza fedha hizo ni sawa na asilimia 72.80 ya bajeti iliyoidhinishwa na kubainisha mafanikio yaliyopatikana hadi kufikia Machi, 2026.

Ulega ameeleza katika Sekta ya barabara, Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) umefanikiwa kukamilisha ujenzi wa kilometa 206.33 za barabara kwa kiwango cha lami pamoja na madaraja makubwa manne. Aidha, miradi 76 kati ya 81 ya dharura ya ujenzi wa madaraja yaliyoathiriwa na mvua za El-Nino imekamilika.

Ulega alibainisha kuwa ujenzi wa madaraja muhimu ikiwemo Pangani, Jangwani, Mbambe, Sukuma, Simiyu, Mirumba na Mitomoni unaendelea katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Kwa upande wa viwanja vya ndege, alisema kuwa awamu ya kwanza ya uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Tabora na Iringa imekamilika, huku ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Msalato ukiwa umefikia asilimia 83. Viwanja vingine vinavyoendelea kujengwa ni pamoja na Sumbawanga na Shinyanga (asilimia 95 kila kimoja), Musoma (asilimia 67) na Kigoma (asilimia 42).

Akizungumzia vivuko, Waziri huyo alisema Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) umekamilisha maegesho ya Bwiro–Bukondo pamoja na Kisoraya–Rugezi–Bukimwi, sambamba na kukamilisha ujenzi wa kivuko cha Kisorya–Rugezi na ukarabati wa boti ya MV Tangazo.

Katika sekta ya majengo ya Serikali, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) unaendelea na ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma katika maeneo ya Magomeni Kota awamu ya pili na Temeke Kota jijini Dar es Salaam, Ghana Kota mkoani Mwanza, pamoja na Kaloleni Kota mkoani Arusha.

Ulega alisisitiza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara ya Ujenzi itahakikisha inatekeleza kwa vitendo maono na dira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea Watanzania maendeleo endelevu kupitia miundombinu bora, salama na yenye tija.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Selemani Kakoso, aliipongeza Wizara hiyo kwa juhudi zake katika kusimamia na kutekeleza miradi ya kimkakati, hususan ujenzi wa barabara na madaraja unaorahisisha usafiri na usafirishaji wa mizigo na abiria nchini.