MRADI WA KIJANISHA DODOMA WAENDELEA KWA KASI, MITI 87,500 YAPANDWA
Dodoma, 22 Machi, 2026
Mradi wa kimkakati wa “Kijanisha Dodoma” unaotekelezwa kwa gharama ya TZS bilioni 12.8 kupitia ufadhili wa GEF na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), unaendelea vizuri tangu kuanza kwake Juni 2024, ukitarajiwa kukamilika Oktoba 2029.
Mradi unasimamiwa na TANROADS kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo TAFORI, TFS, NCC, Jiji la Dodoma, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) na UDOM, ukiwa na jumla ya miradi midogo 12 inayolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Hadi sasa, miradi saba ipo katika hatua mbalimbali, ikiwemo upandaji wa miti 150,000 kando ya barabara ya mzunguko wa nje (km 112.3) ili kuunda ukanda wa kijani. Tayari miti 87,500 imepandwa kwa kushirikiana na JKT Kikosi cha 834 Makutupora, na inaendelea kustawi vizuri, huku miti mingine 25,000 ikitarajiwa kupandwa kabla ya msimu wa mvua kuisha.
Ili kuhakikisha uhai wa miti, mradi utaanzisha mfumo wa umwagiliaji wa matone, huku changamoto ya uharibifu wa miti kutokana na mifugo ikiendelea kushughulikiwa.
Sambamba na hilo, miradi mingine kama uanzishaji wa bustani za Swaswa na Chimwaga, pamoja na maandalizi ya miongozo ya upandaji miti mijini na ujenzi wa kijani, inaendelea kwa mafanikio.
Mafanikio ya mradi huu yanaunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhimiza utunzaji wa mazingira, huku wananchi wakihimizwa kushiriki kikamilifu kulinda na kuendeleza mradi huu kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.