News

TUNDUMA YAFUNGUKA: TANROADS YAPANUA BARABARA KUONDOA FOLENI NA KUCHOCHEA BIASHARA ZA KIMATAIFA

TUNDUMA YAFUNGUKA: TANROADS YAPANUA BARABARA KUONDOA FOLENI NA KUCHOCHEA BIASHARA ZA KIMATAIFA

Katavi

18/03/2026

Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza utekelezaji wa mradi wa kupanua barabara katika mpaka wa Tunduma ili kupunguza msongamano wa magari uliokuwa ukiathiri biashara na usafirishaji katika ukanda wa nchi jirani.

Akizungumza katika eneo la mradi, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe, Mhandisi Frederick Mande, amesema hatua hiyo inatokana na changamoto ya muda mrefu ya foleni kubwa ya magari kutokana na njia finyu ya kuingia mpakani hapo.

“Mkoa wa Songwe unapakana na nchi za Zambia na Malawi, na mpaka wa Tunduma unapokea magari mengi yanayoelekea pia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na nchi za Kusini mwa Afrika. Hali hii ilisababisha msongamano mkubwa,” alisema Mande.

Amefafanua kuwa, awali barabara hiyo ilikuwa na njia moja pekee, hali iliyosababisha magari kupita kwa zamu na kuchelewesha huduma mpakani.

Kutokana na hali hiyo, TANROADS ilitangaza zabuni ya utekelezaji wa mradi huo na kumpata mkandarasi, Marmo Construction Co. Ltd ya mkoani Iringa, ambaye tayari amesaini mkataba na kuanza kazi ya upanuzi wa barabara hiyo.

Mradi huo unahusisha kuongeza njia kutoka moja hadi nne, ambapo magari yataweza kupita kwa njia mbili kwa wakati mmoja, hatua inayotarajiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari.

Kwa mujibu wa Mhandisi Mande, hadi sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 15, huku kazi ikiendelea vizuri bila changamoto za madai kutoka kwa mkandarasi.

Mradi huo unagharimu shilingi bilioni 6.8 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita tangu kuanza kwake.

Mhandisi Mande ameendelea kwa kusema kuwa, ifikapo mwishoni mwa mwezi Julai, mwaka huu, barabara hiyo itakuwa imekamilika na kuanza kutumika, hali itakayorahisisha usafirishaji na kuchochea biashara kati ya Tanzania na nchi jirani.