News

MADARAJA YA KABALISI NA SANGE YAKAMILIKE MACHI 30, KASEKENYA

MADARAJA YA KABALISI NA SANGE YAKAMILIKE MACHI 30, KASEKENYA

Mbeya, 11 Machi, 2026

Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amemtaka mkandarasi JASCO anaejenga daraja la Kabalisi mita 40 na GEMEN anaejenga daraja la Sange mita 40 wilayani Ileje kuhakikisha ujenzi huo unakamilika ifikapo machi 30 mwaka huu.

Mhandisi Kasekenya amezungumzia umuhimu wa ujenzi huo kuendana na uwekaji wa taa katika madaraja hayo na kuhakikisha mitaro karibu na madaraja hayo inasakafiwa vizuri.

"Hakikisheni ujenzi wa madaraja haya unakidhi ubora uliosanifiwa ili kuwiana na barabara za lami zitakapojengwa", amesema Mhandisi Kasekenya.

Msimamizi wa ujenzi huo Mhandisi Jonas Matete kutoka Kitengo cha Usimamizi wa Barabara cha Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) (TECU), amesema atawasimamia Wakandarasi hao ili madaraja hayo yayojengwa sehemu zenye miinuko yakamilike kwa wakati na ubora na hivyo kuchochea fursa za kijamii na kiuchumi kwa wananchi. 

Madaraja ya Kabalisi na Sange yako katika barabara ya mkoa itokayo Ibungu- Kalembo-Kafwafwa hadi Kimo yenye urefu wa km 46.1 na inaunganisha wilaya ya Ileje mkoani Songwe na Rungwe mkoani Mbeya.

Zaidi ya shilingi Bilioni 7.9 zimetumika katika ujenzi wa daraja la Kabalisi wakati shilingi Bilioni 7 zikitumika kujenga daraja la Sange.