News

BARABARA YA LUSAHUNGA - RUSUMO KUCHOCHEA BIASHARA NA UCHUMI WA KANDA

BARABARA YA LUSAHUNGA - RUSUMO KUCHOCHEA BIASHARA NA UCHUMI WA KANDA

Kagera, 10 Machi, 2026

Utekelezaji wa mradi wa ukarabati wa barabara ya Lusahunga – Rusumo unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa wananchi na kukuza biashara kati ya Tanzania na nchi jirani za Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Mwakilishi wa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera, Mhandisi Christian Mbise, amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutapunguza muda wa safari na gharama za usafirishaji, kuongeza usalama barabarani na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kikanda.

Ameeleza kuwa barabara hiyo ni muhimu katika kurahisisha usafirishaji wa mizigo na mazao ya biashara kwa wananchi wa Ngara, Karagwe na maeneo jirani, huku pia ikirahisisha biashara ya mipakani kati ya Tanzania na nchi jirani.

Aidha, amesema wakati wa utekelezaji wa mradi huo takribani ajira 800 zimetolewa kwa wakazi wa maeneo ambayo barabara hiyo inapita.

Kwa niaba ya Menejimenti ya TANROADS, Mhandisi Mbise ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo ya miundombinu ya barabara inayochochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kwa upande wake, Msimamizi wa mradi kutoka NORPLAN Tanzania, Mhandisi Laurent Maganga, amesema licha ya changamoto za mvua za mara kwa mara, mradi huo unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika kwa wakati kama ilivyoainishwa kwenye mkataba.

Naye dereva wa malori anayesafirisha mizigo kati ya Burundi na Rwanda, Bw. Iranzi Cednic, ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kukarabati kipande hicho cha barabara akisema kuwa safari ambazo awali zilikuwa zikichukua muda mrefu sasa zimekuwa rahisi na za haraka zaidi.