News

TANROADS YAENDELEA NA UJENZI WA BARABARA YA LUSAHUNGA - RUSUMO

TANROADS YAENDELEA NA UJENZI WA BARABARA YA LUSAHUNGA - RUSUMO

Kagera, 10 Machi, 2026

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa ukarabati mkubwa wa barabara ya Lusahunga – Rusumo (mpaka wa Tanzania na Rwanda) yenye urefu wa kilometa 92 kwa kiwango cha lami.

Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Mwakilishi wa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera, Mhandisi Christian Mbise, amesema ujenzi huo unatekelezwa na mkandarasi China Civil Engineering Construction Corporation (CCECC) na kusimamiwa na mshauri elekezi NORPLAN Tanzania kwa kushirikiana na kampuni ya TYPSA kutoka Hispania, chini ya kitengo cha usimamizi wa miradi cha TanTIP, kwa ufadhili wa Benki ya Dunia pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mhandisi Mbise amesema mradi huo unaanzia Lusahunga katika Wilaya ya Biharamulo hadi Rusumo katika Wilaya ya Ngara, na kwa sasa umefikia takribani asilimia 50 ya utekelezaji, huku ukitarajiwa kukamilika Desemba 2026.

Amesema mkataba wa ukarabati wa barabara hiyo ulisainiwa tarehe 18 Februari 2023 kati ya Mtendaji Mkuu wa TANROADS na mkandarasi CCECC kwa gharama ya takribani shilingi bilioni 178.4 bila VAT.

Akielezea hatua za ujenzi, amesema ujenzi wa tuta la barabara (Embankment) umekamilika kwa asilimia 100, huku tabaka la chini la msingi (Sub-base) likiwa limefikia asilimia 57. 

Aidha, tabaka la kwanza la lami ya zege (Asphalt Concrete SP 37.5) limefikia asilimia 42.2 wakati tabaka la juu la mwisho (Wearing Course) bado halijaanza kulingana na mpango kazi wa mkandarasi.

Aidha, ujenzi wa makalavati madogo na makubwa umekamilika kwa asilimia 100, huku ujenzi wa njia maalum za magari mazito kwenye maeneo ya mteremko mkali (Climbing Lanes) zenye urefu wa kilometa 25 ukiwa umefikia takribani asilimia 70.