RAIS DKT SAMIA KUIFUNGUA RUKWA KIMIUNDOMBINU
Rukwa, 09 Machi, 2026
Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuifungua nchi kimiundombinu ya barabara, madaraja na viwanja vya ndege, ili kuchochea uzalishaji na biashara mipakani.
Akizungumza na wakazi wa Namanyere Wilayani Nkasi katika ziara ya Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba inayoendelea mkoani Rukwa mhandisi Kasekenya amesema Rais Dkt. Samia ameamua kuwekeza kwenye barabara ili kuwezesha wananchi kufanya shughuli za kijamii na kiuchumi kwa haraka, uhakika na unafuu zaidi.
"Mkoa wa Rukwa ni mkoa wa kimkakati hivyo tumeelekezwa kuwa uwekezaji katika Ziwa Tanganyika uendane na ujenzi wa barabara ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji na hivyo kuchochea uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla", amesisitiza Mhandisi Kasekenya.
Mhandisi Kasekenya amesema Wizara ya Ujenzi imepanga kuzijenga kwa lami barabara za Laela-Kizombwe-Kaseesya Km.136.8; Namanyere- Katongoro-Kapili Port Km 64.80 na Lyazumbi-Kabwe Km 63.85 kwa kiwango cha lami, ili kuchochea biashara kati ya nchi za Tanzania, Kongo na Zambia.
Amezitaja barabara nyingine zitazojengwa ili kuufungua ukanda wa Magharibi mwa Tanzania kuwa ni Kibaoni-Mpanda (Stalike) Km 71; Mpanda-Mishamo Km 100 na Mishamo-Uvinza Km 86.