WAZIRI MKUU DKT NCHEMBA ARIDHISHWA UJENZI KIWANJA CHA NDEGE CHA SUMBAWANGA
Rukwa, 09 Machi, 2026
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mwigulu Nchemba ameipongeza Wizara ya Ujenzi na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Rukwa kwa ujenzi uliozingatia ubora na viwango wa wa Kiwanja cha ndege cha Sumbawanga.
Amesema hayo leo tarehe 09 Machi, 2026 alipokagua maendeleo ya ujenzi huo na kusisitiza kuwa kiwanja hicho kimejengwa kwa viwango vya kisasa.
"Hongereni wana Rukwa kwa kupata kiwanja cha ndege cha kisasa kitakachochochea fursa nyingi za kiuchumi", amesema Dkt. Nchemba.
Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema ujenzi wa kiwanja cha ndege hicho unaotekelezwa na mkandarasi M/s Beijing Construction Engineering Group Co Ltd kutoka China, ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 96 na utakamilika ifikapo April Mosi, 2026.
"Tumejipanga kuhakikisha tunawakabidhi kiwanja hiki wenzetu wa Wizara ya Uchukuzi, maana hadi ifikapo April Mosi kitakuwa kimekamilika kwa kila kitu", amesisitiza Mhandisi Kasekenya.
Mhandisi Kasekenya amesema kazi ya ujenzi wa njia ya kuruka na kutua ndege, barabara za viungio, maegesho ya ndege na jengo la abiria vyote vimeshakamilika.
Naye Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile amesema wako tayari kukipokea kiwanja hicho mapema mwezi ujao ili kuanza kutoa huduma za ndege mkoani humo.
Kiwanja cha ndege cha Sumbawanga ambacho kilijengwa mwaka 1945 na kukarabatiwa mwaka 1985, ambapo sasa kimefanyiwa uboreshaji mkubwa na wa kisasa utakaowezesha ndege za saizi ya kati kutumia kiwanja hicho ambapo zaidi ya shilingi Bilioni 60 zimetumika.