News

TANROADS YATEKELEZA UJENZI WA NJIA NNE KUINGIA MKOANI KAGERA, YAPUNGUZA AJALI NA KUCHOCHEA MAENDELEO

TANROADS YATEKELEZA UJENZI WA NJIA NNE KUINGIA MKOANI KAGERA, YAPUNGUZA AJALI NA KUCHOCHEA MAENDELEO

Kagera, 01 Machi, 2026

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) unaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara kuu ya kuingia mkoa wa Kagera kwa njia nne kwa kiwango cha lami, hatua inayolenga kuongeza usalama barabarani na kuboresha usafiri na usafirishaji katika ukanda huo wa Kanda ya Ziwa.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera, Mhandisi Christian Mbise amesema mradi huo unaanzia katika mzunguko wa Rwamishenye hadi kona ya Mitaga.

Ujenzi wake ulianza mwaka 2023 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2026 kwa gharama ya Shilingi bilioni 5.6.Kwa mujibu wa Mhandisi Mbise, mradi huo ni wa kimkakati, ukilenga kupunguza ajali zilizokuwa zikitokea mara kwa mara katika eneo la mlima wa Nyangoye.

Awali, mlima huo uliokuwa na mwinuko mkali ulisababisha magari mengi ya mizigo kushindwa kupanda na wakati mwingine kurudi nyuma, hali iliyochangia ajali kwa magari madogo na watumiaji wengine wa barabara.

“Mradi huu mkubwa utakuwa chachu ya kuleta maendeleo kwa wakazi wa Kagera kwa ujumla, kwa kuwa utahakikisha usafiri na usafirishaji unakuwa wa uhakika, salama na wa haraka zaidi,” amesema Mhandisi Mbise.

Barabara hiyo itakuwa na njia nne, mbili kwa kila upande, hatua inayotarajiwa kupunguza msongamano wa magari na kuongeza usalama kwa watumiaji wote wa barabara hiyo muhimu inayoingia mkoani Kagera.

Kwa upande wake, Afisa Usafirishaji na dereva wa bodaboda, Bw. Denice Lauriani, ameipongeza Serikali kwa uamuzi wa kupanua barabara hiyo na kuondoa kilima kilichokuwa chanzo cha ajali za mara kwa mara.

“Upanuzi huu utarahisisha usafiri na kupunguza hatari tulizokuwa tunakabiliana nazo kila siku. Tunashukuru Serikali kwa hatua hii,” amesema Bw. Denice.