News

MIRADI YA DHARURA KAGERA YATOA AJIRA NA KUFUFUA SHUGHULI ZA KIUCHUMI

MIRADI YA DHARURA KAGERA YATOA AJIRA NA KUFUFUA SHUGHULI ZA KIUCHUMI

Kagera, 28 Februari, 2026

Kukamilika kwa miradi mitano ya dharura ya madaraja na barabara unganishi mkoani Kagera kumeanza kuleta matumaini mapya kwa wananchi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto za usafiri na usafirishaji kufuatia athari za mvua za El-Niño.

Miradi hiyo iliyotekelezwa na Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mfuko wa CERC, imelenga kurejesha mawasiliano yaliyokatika na kuhakikisha huduma za kijamii na kiuchumi zinaendelea bila vikwazo.

Wananchi wameeleza kufurahishwa na maboresho hayo. Bw. Jaffar Abdul, dereva wa teksi kutoka Kanazi kwenda Mgaza, amesema ujenzi wa Daraja la Kalebe umeondoa adha ya magari kusubiriana kuvuka, kwani sasa magari mawili yanaweza kupishana kwa urahisi tofauti na awali.

Kwa upande wake, Bw. Yassin Abutwa, mfanyabiashara wa ndizi kutoka Kanazi kwenda Mgaza, amesema usafiri wa uhakika utasaidia kupeleka mazao sokoni kwa wakati bila hofu ya kusombwa na maji kama ilivyokuwa hapo awali.

Naye kijana Lameck Samwel, fundi seremala mkazi wa Kyanyabasa, amesema miradi hiyo imetoa ajira kwa vijana wengi waliokuwa hawana shughuli rasmi, na kumwezesha kugharamia mahitaji ya familia ikiwemo ada za watoto na kodi ya pango.

Akizungumza kuhusu ulinzi wa miundombinu hiyo, Mhandisi Christian Mbise amewataka wananchi kuitunza kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo, akionya kuwa yeyote atakayeharibu atachukuliwa hatua za kisheria.

 Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeonesha dhamira ya dhati katika kurejesha na kuimarisha miundombinu ya usafiri mkoani Kagera, hatua inayochochea maendeleo, kuimarisha uchumi wa wananchi na kuunganisha jamii kwa uhakika zaidi