KAGERA YAREJESHA MAWASILIANO BAADA YA KUKAMILISHA MIRADI MITANO YA DHARURA YA MADARAJA
Kagera, 28 Februari, 2026
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kagera imekamilisha miradi mitano ya dharura ya ujenzi wa madaraja, makalavati na barabara unganishi iliyofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mfumo wa mfuko wa dharura (CERC), kufuatia athari za mvua kubwa za El-Niño za mwaka 2023 na 2024. Miradi hiyo imetekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 45.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Mkoa, Mhandisi Christian Mbise amesema miundombinu mingi ya barabara katika mkoa huo ilikatika kutokana na mvua nyingi zinazoambatana na mazingira ya Kagera yenye misitu ya asili na mvua za mara kwa mara. Hali hiyo ilisababisha changamoto kubwa ya mawasiliano kati ya wilaya na vijiji.
Miongoni mwa miradi iliyotekelezwa ni Daraja la Kanoni lililopo Wilaya ya Bukoba Mjini lenye urefu wa mita 30, upana wa mita 18 na barabara unganishi ya mita 600. Mradi huo umefikia asilimia 95 na unatekelezwa na kampuni ya Abemulo Contractors.
Daraja la Kyanyabasa lililopo Wilaya ya Kagera Vijijini lina urefu wa mita 105 na barabara unganishi ya mita 600, likitekelezwa na Gemen Engineering na kufikia asilimia 85 ya utekelezaji.
Wilaya ya Muleba Kusini imenufaika na Daraja la Kamishango lenye urefu wa mita 45 pamoja na barabara unganishi ya kilometa 2, likitekelezwa na D.R.K General Merchant na kufikia asilimia 94.
Daraja la Kalebe lililopo Wilaya ya Bukoba Kusini lina urefu wa mita 60 na barabara za maungio za kilometa 1.5 kwa kiwango cha changarawe, likitekelezwa na Milembe Construction Co na kufikia asilimia 94.
Mradi wa tano ni Daraja la Kyetema lililopo Wilaya ya Bukoba Vijijini lenye urefu wa mita 60 na barabara unganishi ya kilometa 1.0, likitekelezwa na Gemen Engineering na kufikia asilimia 94.
Mhandisi Mbise amesema miradi yote imetekelezwa kwa asilimia 100 na wakandarasi wazawa, hatua iliyochochea ajira kwa Watanzania wengi na kuongeza mzunguko wa fedha katika jamii. Aidha, jumla ya taa 150 zitasimikwa katika maeneo ya miradi hiyo ili kuimarisha usalama wa watumiaji na kulinda miundombinu.
Amesisitiza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutahakikisha upatikanaji wa mawasiliano ya uhakika wakati wote wa masika na kiangazi, na kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi wa Kagera.