BARABARA YA MIKUMI KUJENGWA UPYA KIWANGO CHA ZEGE
Mikumi, 27 Februari, 2026
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) ipo katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi atakayetekeleza ujenzi wa barabara ya Morogoro – Mikumi eneo la mizani (mita 600) kwa kiwango cha zege.
Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia ongezeko kubwa la malori yanayopita katika barabara kuu ya TANZAM Highway, hali inayochangia uchakavu wa haraka wa barabara katika eneo hilo muhimu la mizani.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wake, Waziri Ulega alieleza kuwa ujenzi wa zege utaongeza uimara wa barabara, kupunguza gharama za matengenezo ya mara kwa mara na kuhakikisha mtiririko wa magari unaendelea kwa ufanisi bila usumbufu.
Mbali na ujenzi wa barabara, mradi huo utaambatana na ujenzi wa maegesho ya kisasa ya magari ya mizigo yatakayokuwa ya kulipia, ikiwa ni chanzo cha mapato yatakayochochea shughuli za kiuchumi katika eneo la Mikumi.
“Tutatengeneza maegesho mazuri ili kuwe na utaratibu, lakini pia iwe fursa ya kibiashara, watakaoegesha magari yao watalipa na hivyo kuchangia kukuza uchumi wa Taifa,” amesema Waziri Ulega.
Aidha, amesisitiza kuwa utekelezaji wa mradi huo utaenda sambamba na uwekaji wa taa za barabarani, kufuatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba miradi ya barabara iunganishwe na miundombinu ya mwanga ili kuwezesha shughuli za kiuchumi kufanyika mchana na usiku.
Kwa kuwa Mikumi ni kitovu muhimu cha biashara na usafirishaji, maboresho hayo yanatarajiwa kuimarisha usalama, kuongeza ufanisi wa usafiri wa mizigo na kufungua zaidi fursa za biashara kwa saa 24, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi wa eneo hilo na Taifa kwa ujumla.