BUGENE-BURIGI CHATO: BARABARA YA FURSA KAGERA YAPIGA HATUA KWA KASI
Kagera, 27 Februari, 2026
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kagera unaendelea kwa kasi na ujenzi wa barabara ya kimkakati ya Bugene – Hifadhi ya Taifa ya Burigi Chato yenye urefu wa kilometa 60, ambapo utekelezaji umefikia asilimia 46.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Mwakilishi wa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera, Mhandisi Christian Mbise, amesema barabara hiyo ya kiwango cha lami ni sehemu ya mradi mpana wa Bugene – Kasulo (Benaco) – Kumunazi (Km 128.5) unaoanzia Kata ya Bugene, Wilaya ya Karagwe na kuishia ndani ya hifadhi hiyo.
Ujenzi unatekelezwa na Mkandarasi China Road and Bridge Corporation (CRBC) kwa kuzingatia viwango vya juu vya ubora ili kuhakikisha inadumu na kuhudumia ongezeko la mahitaji ya usafiri na biashara.Barabara hiyo ni kiungo muhimu kinachounganisha Tanzania na nchi jirani za Uganda, Burundi na Rwanda, huku ikiwa mhimili wa usafirishaji kwa wilaya za Kyerwa, Karagwe, Misenyi na Ngara.
Kukamilika kwake kutarahisisha kwa kiasi kikubwa usafirishaji wa mazao ya biashara kama kahawa, parachichi na ndizi, pamoja na mifugo, samaki na malighafi nyingine kwenda masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Huu ni mradi wa kimkakati unaolenga kufungua fursa mpya za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Kagera na Taifa kwa ujumla kupitia miundombinu imara ya barabara,” amesema Mhandisi Mbise.
Kupitia barabara hiyo inayopita katika ukanda wa hifadhi, sekta ya utalii inanufaika zaidi kwa kuwawezesha watalii kufika kwa urahisi na kwa wakati, hali inayotarajiwa kuongeza mapato na kuchochea uwekezaji katika eneo hilo.
Aidha, usanifu wa kisasa umeondoa changamoto za vilima na maeneo korofi yaliyokuwa yakisababisha magari kukwama wakati wa mvua, hivyo kuboresha usalama na kupunguza ucheleweshaji wa safari.Serikali imeufadhili mradi huo kwa asilimia 100 kwa fedha za ndani, hatua inayodhihirisha dhamira ya kuimarisha uchumi kupitia uwekezaji katika miundombinu.
Mkandarasi amelipwa kwa wakati, ambapo hadi sasa zaidi ya Shilingi bilioni 22 tayari zimelipwa, jambo linaloendelea kuupa kasi utekelezaji wa kazi.