DARAJA LA MASUMBWE- MWABOMBA LAONDOA ADHA YA MITUMBWI NA GHARAMA KWA WANANCHI GEITA
Geita, 25 Februari, 2026
Katika mradi mwingine wa dharura chini ya utaratibu wa mfuko wa CERC, TANROADS imekamilisha ujenzi wa daraja kubwa katika eneo la Masumbwe hadi Mwabomba, linalounganisha Wilaya za Mbogwe na Ushetu.
Awali, daraja la zamani lilikuwa likijaa maji na kulazimisha wananchi kuvuka kwa mitumbwi kwa gharama kubwa. Sasa serikali imejenga daraja jipya lenye midomo 15 inayopitisha maji mengi, hatua iliyomaliza kabisa changamoto ya mafuriko kupita juu ya barabara.
Mhandisi Mkazi wa mradi, Mhandisi Kaluge Masele, ameishukuru serikali kwa kutoa fedha kwa wakati, zilizowezesha kukamilika kwa mradi huu muhimu wa kuunganisha wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mwabomba, Bw. Juma Ligula, amesema kukamilika kwa daraja hilo kutaongeza chachu ya maendeleo hasa kwa kuzingatia uwepo wa soko la dhahabu linalochimbwa na wachimbaji wadogo katika kijiji hicho, pamoja na kurahisisha usafirishaji wa mazao na mifugo.
“Ninawashukuru pia wawakilishi wa Mbogwe na Ushetu kwa kuisemea barabara hii. Sasa tuna uhakika wa usafiri hata wakati wa mvua,” amesema Bw. Juma, huku akitoa wito kwa wananchi kulinda miundombinu hiyo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake, Bi. Esther Peter, mama lishe katika eneo la Mwabomba, amesema ujenzi wa daraja hilo umemsaidia kuongeza kipato chake, kwani awali alitumia gharama kubwa kwa usafiri wa bodaboda na mtumbwi kufuata mahitaji ya chakula.
“Sasa nalipa kodi ya nyumba na watoto wangu wanasoma kutokana na kipato ninachopata hapa,” amesema.
Nao waendesha bodaboda Bw. Boniface Rahama na Paul Mwasunga wamesema sasa wanavuka kwa urahisi bila hofu ya maji mengi, tofauti na ilivyokuwa awali walipokwama upande mmoja wa daraja.
Kukamilika kwa miradi hii miwili kunadhihirisha dhamira ya serikali ya kuimarisha miundombinu, kulinda uchumi wa wananchi na kuhakikisha barabara zinapitika majira yote ya mwaka.