News

TANROADS YAFUNGUA RASMI NJIA YA BIASHARA KATI YA TANZANIA NA RWANDA            

TANROADS YAFUNGUA RASMI NJIA YA BIASHARA KATI YA TANZANIA NA RWANDA            

Geita, 25 Februari 2026

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Geita imekamilisha ujenzi wa sehemu muhimu ya barabara kuu ya Wendele – Mlele inayounganisha Tanzania na Rwanda, kwa kujenga makalavati tisa (9) na kunyanyua tuta la barabara katika maeneo ya Kanegere na Lubeho yaliyokuwa yameathirika na mvua za El-Nino za mwaka 2023 – 2024.

Akizungumza kuhusu mradi huo, Mhandisi Mkazi wa mradi, Mhandisi Kaluge Masele, amesema kazi hiyo imefanyika kwa kuzingatia viwango na ubora wa kitaalamu, ikihusisha jumla ya kilometa 2.9 - ambapo Km 1.5 ni Kanegere na Km 1.4 ni Lubeho.Katika eneo la Kanegere yamejengwa makalavati makubwa saba, huku Lubeho yakijengwa mawili.

Miongoni mwa makalavati hayo, yapo yenye midomo mitatu na jingine lenye midomo miwili, hatua iliyochukuliwa kukabiliana na changamoto ya maji kupita juu ya barabara na kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji waliolazimika kusubiri maji kupungua.

Kwa sasa utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 99, ambapo kazi zilizobaki ni uwekaji wa alama za usalama barabarani na uimarishaji wa kingo kwa mawe maalum ili kuzuia mmomonyoko wa udongo.

“Kazi inayoendelea ni kukamilisha uwekaji wa alama za usalama na kuimarisha tuta kwa pembeni kwa mawe hadi kwenye makalavati ili kulinda miundombinu dhidi ya mvua,” amesema Mhandisi Masele.

Kukamilika kwa mradi huu kunatarajiwa kuimarisha usafirishaji wa mizigo kati ya Tanzania na Rwanda, hasa kwa magari makubwa yanayotumia njia hiyo kama sehemu ya mtandao wa biashara wa kikanda.