News

TANROADS YAENDELEA NA UJENZI WA BARABARA YA KIMKAKATI INAYOUNGANISHA MIKOA YA SINGIDA NA MBEYA

TANROADS YAENDELEA NA UJENZI WA BARABARA YA KIMKAKATI INAYOUNGANISHA MIKOA YA SINGIDA NA MBEYA

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Singida inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kimkakati wa ujenzi wa barabara ya Mbeya – Makongolosi – Manyoni (Mkiwa) yenye urefu wa kilometa 510.80, inayounganisha Mikoa ya Mbeya na Singida pamoja na maeneo ya kati ya nchi.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida, Mhandisi Dastan Singano amesema mradi huo unatekelezwa kwa awamu saba, kuanzia Mbeya kupitia Chunya, Makongolosi, Rungwa, Itigi hadi Mkiwa.

Kwa upande wa Mkoa wa Singida, ujenzi unaendelea katika kipande cha Sehemu ya Saba A (Lot 7A) chenye urefu wa kilometa 25. Kati ya hizo, kilometa 20 tayari zimekamilika kwa kiwango cha lami, huku kilometa tano zilizobaki zikitarajiwa kukamilika ifikapo Mei 2026.

Ameeleza kuwa Sehemu ya 7A inaanzia Noranga (Doroto) hadi Itigi (Mlongoji) kwa gharama ya Shilingi Bilioni 29.054, ikihusisha pia ujenzi wa kalavati kubwa moja na makalavati madogo kadhaa. Sehemu ya 7B itaanzia Itigi Roundabout hadi Mkiwa kwenye makutano na barabara ya Dodoma – Manyoni – Singida – Shelui – Nzega.

Mradi huu unatekelezwa na mkandarasi CHICO kwa fedha za ndani, ambapo hadi sasa utekelezaji wa Sehemu ya 7A umefikia asilimia 80.31.

Kukamilika kwa barabara hii kunatarajiwa kurahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa za kilimo, misitu, ufugaji na uvuvi, kuimarisha mtandao wa usafirishaji kati ya mikoa ya kati na nyanda za juu kusini, pamoja na kuwezesha biashara na nchi jirani za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, DRC, Zambia na Malawi.

Aidha, TANROADS ina mpango wa kusimika taa katika maeneo ya vijiji vitakavyoonekana kustahili ili kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara na miundombinu yake.

Mhandisi Singano ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya miundombinu ya barabara nchini, huku akiwahimiza wananchi na watumiaji wa barabara hiyo kuitunza miundombinu ikiwemo alama za barabarani, madaraja na makalavati ili iweze kudumu kwa muda mrefu.