TANROADS YASAIDIA JAMII KWA KUJENGA MADARASA, KITUO CHA AFYA NA NYUMBA YA MWALIMU MKUU – SINGIDA
Singida, 20 Februari, 2026
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Singida imejitolea kusaidia jamii kwa kujenga miundombinu muhimu katika Vijiji vya Nkonkilangi na Ntwike, kupitia Mradi wa Dharura wa ujenzi wa Daraja la Nkonkilangi.
Msaada huo umetolewa baada ya daraja kuharibika kutokana na mafuriko ya mvua za El Niño za mwaka 2023 na 2024.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida, Mhandisi Dastan Singano, amesema msaada huo umejumuisha ujenzi wa madarasa mawili, Kituo cha Afya, Zahanati, na kukamilisha nyumba ya Mwalimu Mkuu.
Aidha, mradi huo umechangia kuchonga barabara tatu za vijijini, moja katika Kijiji cha Nkonkilangi (km 3) na mbili katika Kijiji cha Ntwike (km 2 kila moja).
TANROADS pia imechangia mifuko ya saruji 60 kwa ujenzi wa soko Ntwike, mifuko 15 kwa choo cha Shule ya Sekondari Ntwike, na mchanga mita za ujazo 300 kwa Kituo cha Afya Ntwike. Pia wamechangia shilingi 7,680,000 kukamilisha nyumba ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Sekenke, pamoja na kifusi na mchanga kwa ajili ya Kituo cha Afya Nkonkilangi.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Sekenke, Bw. Basil Mussa, ameishukuru Serikali kwa daraja hilo kubwa ambalo limeondoa adha ya wanafunzi kufika shuleni wakati wa mvua. Amesema sasa wanafunzi wanavuka kwa wakati, hali inayoongeza ufaulu na uandikishaji.
Pia ameishukuru TANROADS kwa kukamilisha nyumba yake, hivyo kuwa karibu na shule.
Afisa Elimu Kata ya Ntwike, Bi. Wansilekula Mlewa, amesema msaada huo umesaidia wanafunzi kuingia madarasani bila kukosa, akitaja pia msaada wa vifaa vya michezo uliowasaidia kurudisha baadhi ya watoto shuleni.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Nkonkilangi, Bi. Halima Amasi, amesema kukamilika kwa vituo vya afya kutapunguza umbali wa wananchi kufuata huduma za matibabu.
Ujenzi wa Zahanati ya Nkonkilangi na Kituo cha Afya cha Ntwike umekaribia hatua ya lenta, huku madarasa mawili ya Shule ya Msingi Mapinduzi yakipigwa mbao za kenchi.
Utekelezaji wa mradi huu unaendelea kuimarisha maendeleo ya kijamii kupitia barabara, afya, na elimu.